Wednesday, January 11, 2017

WEKEZA KATIKA UIMARA WA NDANI

Nyumba imara ni ile yenye msingi imara. Msingi mara nyingi hufukiwa chini lakini ndio uimara wa jengo zima ulipo. Vivyo hivyo uimara wako kwa mambo yanayoonekana unatokana na uimara wako wa ndani, uimara wa nafsi. Japo nje waweza onekana imara lakini kipimo pekee cha uimara wako wa ndani ni mtikisiko.

Mtikisiko mkubwa utakaopata ni pale ambapo misingi yako ya ndani itatikiswa. Pale ambapo utawekwa katika mazingira ambayo yatakubidi upime mitazamo yako, upime sheria zako, upime utaratibu wako na kuu kuliko yote upime utambulisho wako. Na ndio maana katika kipindi cha mtikisiko unaweza poteza dira ya utambulisho wako, imani yako na hata utaratibu wako.

Mtikisiko unapoingia lazima uingie uzito wakati huo huo inaingia hali ya hamaki na taharuki. Hapo ndipo utajikuta unafanya maamuzi ambayo hayana faida kwako, hapo utajikuta unaingiwa na ukungu katika macho yako ya ndani ya maono yako.

Hali hiyo ni ya kawaida hasa pale unapotoka katika mfumo mmoja kwenda mwingine, kawaida moja kwenda nyingine. Pale unapotaka kuishi mitazamo yako na ndoto zako kwa mkupuo. Pale unapotaka kukimbia kabla hujapasha joto miguu kwa kutembea. Ni vema ukapasha joto miguu yako na kufurahia kabla hujaanza kukimbia.

Uhuru wa nafsi unahitaji nidhamu na maono yaliyo sambamba na uhalisia. Jaribu kwenda kwa utaratibu lakini ukiwa na uharaka wa kifikra kuchukua maamuzi. Kuwa muwazi juu ya hali yako na utafute watu wachache ambao watakuchoma sindano ya hamasa na watakuamini. Ambao wako tayari kusimama na kukupa moyo.

Unaweza kujiimarisha kwa kuendelea kujipa hamasa na kuwa na fikra chanya, ukichukulia kila changamoto kama njia ya kujiimarisha. Usitafute kujipa kisingizio kama unajua unaweza kujiimarisha. Kila wakati ongeza nguvu yako ya ndani kwa kusimama tena hata kama umechoka. Misuli huja kwa kuongeza zaidi, kujiinua zaidi na kuamini ipo siku mambo yatakuwa mazuri.

No comments:

Post a Comment