Tuesday, June 20, 2017

ITAJIRISHE NAFSI YAKO

Nafsi yako ni hazina kubwa maana ndio kiunganishi cha mwili wako na uhai wako au tunaweza sema roho yako. Nafsi yenye nguvu ni ile inayoweza kudhibiti fikra na kuratibu hisia na kuziweka katika mfumo utakaoleta tija katika maisha na tija kwa yale yanayokuzunguka.

Nafsi imara ni ile inayoweza kuchuja fikra na mawazo na kuhakikisha yanaleta mguso chanya kwa hisia ili zilete msukumo wa utendaji. Huwezi kuwa na nafsi imara kama haudhibiti fikra zako na kama hauratibu hisia zako. Hisia zinatakiwa zipokee msukumo chanya kutoka katika fikra zilizoratibiwa vizuri.

Utatu wa kinafsi yaani hisia, akili na utashi unahitaji kuchunguzwa na kila mwenye nafsi. Inapaswa kama binadamu uhakikishe sheria au misingi ya imani yako imejikita kujenga nafsi imara na sio nafsi dhaifu. Je ni mambo gani yanaingia zaidi katika nafsi yako, je watu wanaokuzunguka wana mguso upi katika nafsi yako? Hayo mambo ni ya kuchunguza sana.

Waweza kuitajirisha nafsi yako kiasi cha kwamba ikawa inatoa misimamo na hisia zenye uwiano, ni jambo lenye changamoto pale akili yako na hisia zikawa na mgongano katika namna inavogusa watu. Utashi wa kimawazo usio na utashi wa kihisia siku zote hauleti matokeo sawa. Unaweza kuwa na utashi wa kimawazo ila pasipo na utashi wa kihisia ukasababisha maafa makubwa.

Je mawazo yako yanaleta mguso gani wa kihisia. Waweza jua jambo lakini ukaliwasilisha likasababisha maafa au hata maudhi. Tajirisha nafsi yako kiasi cha kwamba utashi wako wa kiakili uuwiane na utashi wako wa kihisia. Nikupe mfano wa zawadi, ukipeleka zawadi kwa mtu na umeinunua kwa gharama siku zote lazima uifunge katika boxi la zawadi na uliwekee gift paper. Vivyo hivo ukiwa unatoa madini ya mawazo, ushauri na marekebisho lazima utumie utashi wa kihisia ili anayepokea afurahishwe na kuguswa na zawadi yako.

Hata Kama zawadi ulioifunga sio nzuri sana ila namna ulivoifunga inaweza ikamgusa mtu na akaipokea.

Tajirisha nafsi yako kwa kuweka uwiano katika ukuaji wa utaahi wa kihisia na utashi wa kiakili