Showing posts with label Purpose. Show all posts
Showing posts with label Purpose. Show all posts

Tuesday, June 20, 2017

ITAJIRISHE NAFSI YAKO

Nafsi yako ni hazina kubwa maana ndio kiunganishi cha mwili wako na uhai wako au tunaweza sema roho yako. Nafsi yenye nguvu ni ile inayoweza kudhibiti fikra na kuratibu hisia na kuziweka katika mfumo utakaoleta tija katika maisha na tija kwa yale yanayokuzunguka.

Nafsi imara ni ile inayoweza kuchuja fikra na mawazo na kuhakikisha yanaleta mguso chanya kwa hisia ili zilete msukumo wa utendaji. Huwezi kuwa na nafsi imara kama haudhibiti fikra zako na kama hauratibu hisia zako. Hisia zinatakiwa zipokee msukumo chanya kutoka katika fikra zilizoratibiwa vizuri.

Utatu wa kinafsi yaani hisia, akili na utashi unahitaji kuchunguzwa na kila mwenye nafsi. Inapaswa kama binadamu uhakikishe sheria au misingi ya imani yako imejikita kujenga nafsi imara na sio nafsi dhaifu. Je ni mambo gani yanaingia zaidi katika nafsi yako, je watu wanaokuzunguka wana mguso upi katika nafsi yako? Hayo mambo ni ya kuchunguza sana.

Waweza kuitajirisha nafsi yako kiasi cha kwamba ikawa inatoa misimamo na hisia zenye uwiano, ni jambo lenye changamoto pale akili yako na hisia zikawa na mgongano katika namna inavogusa watu. Utashi wa kimawazo usio na utashi wa kihisia siku zote hauleti matokeo sawa. Unaweza kuwa na utashi wa kimawazo ila pasipo na utashi wa kihisia ukasababisha maafa makubwa.

Je mawazo yako yanaleta mguso gani wa kihisia. Waweza jua jambo lakini ukaliwasilisha likasababisha maafa au hata maudhi. Tajirisha nafsi yako kiasi cha kwamba utashi wako wa kiakili uuwiane na utashi wako wa kihisia. Nikupe mfano wa zawadi, ukipeleka zawadi kwa mtu na umeinunua kwa gharama siku zote lazima uifunge katika boxi la zawadi na uliwekee gift paper. Vivyo hivo ukiwa unatoa madini ya mawazo, ushauri na marekebisho lazima utumie utashi wa kihisia ili anayepokea afurahishwe na kuguswa na zawadi yako.

Hata Kama zawadi ulioifunga sio nzuri sana ila namna ulivoifunga inaweza ikamgusa mtu na akaipokea.

Tajirisha nafsi yako kwa kuweka uwiano katika ukuaji wa utaahi wa kihisia na utashi wa kiakili

Thursday, March 16, 2017

KUWA NA UHUSIANO NA UHALISIA WAKO

Kila binadamu ana uhalisia wake na utofauti wake, binadamu wanaweza fanana tabia lakini kuna msingi wa ndani kabisa wa kinafsi unaowatofautisha. Huu msingi wa kinafsi ndio uhalisia wa yule mtu. Mtu yeyote anayetoka katika uhalisia wake anapoteza utambulisho wake na akipoteza utambulisho wake anapoteza mambo mengi ya kinafsi yaliyomo ndani yake maana inambidi atafute uhalisia mwingine na alazimike kuishi katika uhalisia huo.

Kuna mambo mengi ya kinafsi ambayo mtu hupoteza na kuu kuliko yote ni amani ya nafsi na furaha ya ndani. Hapo ndipo unakutana na mtu ana kila kitu lakini hana furaha wala amani, yamkini kuna mambo kadha wa kadha yanayomtatiza lakini kuu kuliko yote ni kupoteza uhalisia wake. Kuna mambo yanayompa mtu ujasiri wa ndani, kuna misingi ya kinafsi ambayo mtu anakuwa nayo inayompambanua. Akipoteza hivo vitu au akitoka nje ya hivo vitu utaona mabadiliko yake kimtazamo na hata kihisia.

Katika uratibu wa kihisia na kutengeneza uimara wa kihisia mtu lazima arudi katikà uhalisia wake. Watu wengi wamepoteza dira katika mambo mengi kwasababu walitoka katika uhalisia wao ndipo wanakuja kushtuka wameshapotea na wakajikuta wanaishi kama wahanga wa mambo pasipo kujua nini cha kufanya.

Jitambue na jitambulishe na jiimarishe katika uhalisia wako maana utakapokuja kutoka katika uhalisia huo utajaribu kuwa kitu au mtu ambaye haumuelewi hata wewe. Unakuwa kama mtu usiyejitambua, Rudi katika uhalisia wako ili urudishe ile morali na msukumo na msisimko wa ndani kufanya mambo.

Ukiwa katika uhalisia wako mazingira ndo yatalazimika kuendana na uhalisia wako lakini tofauti na hapo wewe ndo utalazimika kuendana na mazingira. Uhalisia hukupa wewe uhuru wa kujipambanua na kujiwasilisha katika jamii ili uwe na mguso chanya. Uhalisia wako ndio hupelekea wewe kutambua kusudi lako na hata kuongeza thamani yako ili ulitende kusudi lako. Hivo ni muhimu sana kuwa katika uhalisia wako.

Jamii au mazingira yasikufanye upoteze uhalisia wako. Jamii ndo inapaswa ipishe njia ili uhalisia wako uweze kuwa na mguso na hii itawezekana tu ukisimama katika kulinda uhalisia wako

Monday, October 3, 2016

TAMBUA UNACHOTAKA KATIKA MAISHA

Moja ya changamoto kubwa ambayo watu wengi huwa tunayo ni kutofahamu nini tunachotaka au tunachohitaji katika maisha. Watu wengi hudhani wanajua wanachokitaka au wanachokihitaji lakini ukiangalia matendo yao utatambua kuwa wengi hawajui wanachokitaka katika maisha. Usipojua unachotaka katika maisha utakuwa ni mtu wa kuzunguka zunguka kujaribu jaribu kila kitu kuona kina mguso gani kwako.

Kuna dhana nyingi sana ambazo tunazo ju ya yale tunayotaka katika maisha na unaweza ukapewa kila ulichodhani unakitaka kisha ukaja kugundua kuwa bado kuna kitu kingine unachokitaka. Na utakuwa ni mtu usiye na furaha wala amani kwasababu hujui unachokitaka. Pengine hata ukawa mtu mwenye lawama katika kila jambo kwasababu wewe mwenyewe hujui unachokitaka.

Pengine pia unaweza jua unachokitaka lakini unadhani ni jambo la kufikirika, huo mtazamo unaweza kukufanya ukaendelea kuwa kama mtumwa anayezunguka jangwani asijue anapoelekea. Kuna mwanafilosofia mmoja aliwahi kusema kuwa Watu wengi hawajui wanachokitaka hadi uwaonyeshe wanachokitaka. Ni muhimu sana kujua unachokitaka.

Njia pekee ya kujua unachokitaka ni kujitathmini nafsi yako na kujitambua utu wako ndipo utajua ni nini unachohitaji. Mwanafilosofia mmoja aliwahi kusema kuwa kama hakuna adui ndani adui wa nje hawezi kutudhuru. Nafsi yako ya ndani imeundwaje? Pengine ushawahi kujiuliza ni jambo gani linakupa amani na unaamini ndio jambo ambalo ukilipata kama msingi wa maisha yako utaweza kupata mambo mengine yote?

Kila nafsi inahitaji uhuru na amani na furaha na wengi wetu tumedhani tukipata vitu basi nafsi yetu ndo itakuwa imepata inachotaka. Hapana!! Nafsi yako inahitaji kukua na jambo lolote linaloweza kuinyanyua nafsi yako ndilo jambo unalohitaji. Nafsi yako inahitaji thamani na jambo linaloweza kuipa thamani nafsi yako ndilo unalohitaji. Nafsi yako inahitaji amani na jambo lolote linaloweza kukupa amani ya nafsi ndilo unalohitaji.

Ukishajua msingi hasa wa mahitaji ya nafsi yako itakuwezesha kutambua ni nini unachohitaji katika maisha, iwe ni katika uchaguzi wa kazi, iwe ni katika mahusiano au nyanja yeyote ya maisha. Utatambua marafiki wa nafsi yako, utatambua hata mwenzi wa nafsi yako, utatambua hata kusudi la maisha yako.

Saturday, September 17, 2016

JENGA MSUKUMO WA NDANI

Binadamu yeyote hutenda mambo kutokana na msukumo fulani. Misukumo iko ya aina mbili. Kuna msukumo wa nje na msukumo wa ndani. Watu wengi hutenda mambo kutokana na msukumo wa nje ambao unahusisha mazingira fulani au faida na matokeo fulani. Sio jambo baya kuwa na misukumo ya nje inayopelekea wewe kutenda jambo lakini changamoto ni kwamba ukiwa na msukumo wa nje zaidi inaweza pelekea kuwa na mguso tofauti.

Misukumo ya nje inaweza kubadilika muda wowote na hii itakupelekea kupoteza kabisa ile ari ya utendaji. Unaposukumwa kutenda jambo kwa ajili ya faida fulani itapelekea kuwa na hamaki pale hasara inapokuja au kukosekana kwa faida husika. Ukisukumwa zaidi na mazingira jua hayo mazingira yanaweza kubadilika muda wowote mfano unaweza pangiwa kutoka Dar es salaam kwenda dodoma. Hii itakusumbua sana katika kupata uwiano wa kihisia.

Ni muhimu kujenga msukumo wa ndani uliojengwa katika msingi wa mambo matatu..Moja ni Uongozi wa maisha yako, Thamani na mwisho ni kusudi.

Uongozi wa maisha yako ni msukumo wa ndani ulio na mtazamo na uthibiti wa muelekeo wa maisha yako. Ukijua ya kwamba wewe ndio mwenye jukumu ya kutengeneza muelekeo wa maisha yako itakupa msukumo wa utendaji kwa maana utajua kila wakati kuwa unalolifanya linatengeneza muelekeo wa maisha yako.

Thamani ni msukumo wa ndani uliojijenga katika mtazamo kuwa kila jambo unalolitenda unalifanya ili likujengee uwezo na ufanisi, likufanye mtu mwenye uwezo zaidi na mwenye ufanisi zaidi...uwe mtu wa thamani na bora. Ndio maana faida kubwa katika kazi sio unachokipata baada ya kazi bali ni unavokuwa baada ya kazi ( Thamani yako)

Kusudi ni msukumo wa jambo uliojijenga katika mtazamo kuwa unafanya jambo kwasababu lina maana kwako na jamii inayokuzunguka. Utasukumwa kufanya jambo kwa sababu lina maana kubwa ndani yako na kwa jamii yako.

Ukiwa na misukumo hiyo mitatu ya ndani katika kila jambo ulifanyalo, kila siku utakuwa na ari na msisimko kufanya mambo na hautopoteza hamu ya kuamka asubuhi kuiendea siku kwa furaha.

Tuesday, September 6, 2016

TENGENEZA UTARATIBU WA KIUONGOZI WA MAISHA YAKO

Pasipo utaratibu mambo huenda mrama. Pasipo uongozi thabiti lazima kuwe na machafuko. Ili uweze kuwa na uthibiti katika maisha lazima kuwe na utaratibu na lazima kuwe na uongozi thabiti. Wewe ni kiongozi wa maisha yako.

Usipokuwa na uongozi binafsi na utaratibu wako wa utendaji lazima utakuwa mtumwa wa uongozi na utaratibu wa mwingine. Mikwaruzo hutokea pale mamlaka zinapokinzana. Pale ambapo kunakosekana uwiano baina ya uongozi binafsi na uongozi unaokuzunguka. Pale ambapo kunakosekana uwiano baina ya utaratibu binafsi na utaratibu unaokuzunguka.

Usipokuwa kiongozi wa maisha yako utawapa wengine fursa ya kushinikiza mambo katika maisha yako na hii itakujengea hali ya kukosa furaha kwa maana utakuwa unashindana na nafsi yako inayotaka kuwa kiongozi lakini imekosa utaratibu wa kiungozi.

Uhuru siku zote una gharama, Huwezi kuwa huru kama unaogopa gharama ya kuwa huru. Nafsi yako inataka kuwa huru lakina usipojenga utaratibu na uongozi wa ndani wa hisia na maamuzi ni vigumu sana nafsi yako kuwa huru.

Je unawezaje kujenga utaratibu na uongozi wa maisha yako:-
1. Usisimame katika msingi wa hisia: siku zote ili kuwa na utaratibu na uongozi katika maisha lazima ujenge msingi imara katika nafsi yako. Na hisia sio msingi imara maana hisia hubadilika kila wakati, huwezi kuwa kiongozi wa maisha yako kama unaenda kwa hisia. Ukienda kwa hisia utajikuta unaendelea kuvipa nafasi vitu ambavyo havitakiwi kupewa nafasi kwa wakati huo.

2. Ongeza maarifa na ufahamu : Huwezi kuwa huru na kuwa kiongozi wa maisha yako kama ufahamu na maarifa yako vina ukomo. Hakuna jambo baya kama uhuru na ujinga. Huwezi kuwa mjinga halafu ukawa kiongozi wa maisha yako. Ujinga ni utumwa ndio maana kuna maandiko yanasema Utaijua kweli nayo kweli itakufanya huru.

3. Tengeneza sheria za maisha yako: lazima utengeneze msingi mgumu tofauti na hisia. Ukishakuwa na maarifa tengeneza sheria zako mwenyewe na hakikisha huzivunji sheria hizo maana ni changamoto na itakuumiza zaidi pale unapovunja sheria zako mwenyewe.

4. Fanya vitu kulingana na vipawa na karama zako : Huwezi kuwa kiongozi bora wa maisha yako kama haujipambanui na wengine. Usiwe mtu wa kufata upepo...Zig ziglar alishawahi kusema kuwa Uongozi sio kufuata njia iliyopitwa na watu bali ni kutafuta njia yako na kuacha alama. Ukiwa mtu wa kujilinganisha na wengine huwezi kuwa na utaratibu wako mwenyewe.

5. Jiamini : Dhana ya kujiamini ni pana sana. Katika jambo lolote lile usipojiamini huwezi fanya chochote, jiamini katika maamuzi yako, jiamini katika unayofanya. Wengi wanashindwa hata kufanya maamuzi magumu kwasababu ya kukosa kujiamini. Kama unataka kuwa kiongozi wa maisha yako jiamini ikiwemo huweze kufanya maamuzi na kuwa tayari kuwajibika kutokana na maamuzi yako.

* Hakuna jambo litakalokupa amani na furaha kama kutambua kuwa una uthibiti wa maisha yako. Ni jambo litakaloongeza ari ya utendaji wako na pia kukupa morali na msisimko wa kila siku wa maisha.

Sunday, August 28, 2016

HAKUNA AJALI, KILA JAMBO LINA KUSUDI

"Huwa hakuna ajali.. Bali kuna kusudi ambalo bado hatujalitambua "-Deepak Chopra

Katika moja ya mafundisho yake mhamasishaji na mkufunzi wa maswala ya kujitambua Deepak chopra alisema huwa hakuna ajali bali kuna kusudi ambalo bado hatujalitambua. Kauli hii ni yenye mtazamo chanya hasa pale tunapokosa majibu ya baadhi ya maswali tuliyonayo katika maisha.

Siku zote kusudi la jambo hufungwa katika muda na maarifa. Kuna usemi ambao wengi wetu huwa tunao hasa pale tunapokosa majibu huwa tunasema limetokea la kutokea tukiweka mtazamo kwamba jambo ilo ni kama muujiza au limetokea kutoka hali ya kutokuwepo. Lakini inatupasa tubadili mitazamo.

Katika kila jambo tusilopata majibu tutambue kuwa kuna kusudi ambalo halijadhiirishwa bado kwa wakati huo hivo inatupasa kutambua yatupasa kuwekeza katika kujikuza kimaarifa huku tukiendelea kutambua kuwa muda muafaka tutakuwa watu wenye ufahamu zaidi juu ya yale yanayotokea.

Hakuna jambo linalotokea kwa ajali...lazima kuwe na kusudi...iwe ni kukukumbusha jambo, kukufundisha jambo au kukuimarisha katika jambo. Lakini ni lazima tujenge tabia ya uvumilivu hadi pale tunapopata maarifa mapana ya jambo hilo.

Muda mwingi tumekuwa ni watu wa kuchukua maamuzi bila maarifa yeyote tunapokuwa katika hali ya kukosa ufahamu juu ya kusudi fulani. Inabidi turuhusu muda na kukua katika maarifa.Kuna ambao wanajifunga katika makubaliano baada ya dakika kumi na tano za hisia kali bila kuruhusu muda kupoza hisia hizo na kupata maarifa juu ya kusudi hilo kabla hawajachukua maamuzi.

Chukua muda wako vizuri huku ukikua ktk maarifa kutambua kusudi la jambo maana hakuna jambo linalotokea kama ajali.

Sunday, August 21, 2016

MSISIMKO WA MAISHA

Je umekosa msisimko wa maisha? Jizamishe katika kazi unayoiamini kwa moyo wako wote, iishi kazi hiyo, na utapata furaha ambayo haukuidhania-Dale Carnegie

Moja ya changamoto kubwa kwa watu sasa hivi ni kukosa msisimko na msukumo wa maisha, Moja ya viashiria vya kukosa msisimko wa maisha ni upweke, lawama na kukosa msukumo wa kufanya mambo. Watu wanakosa ile furaha ya kuamka jumatatu asubuhi, wengine hadi wanaingiwa na hisia hasi ikifika jumapili jioni.

Changamoto hii inatokana na mazoea ya watu ya kufanya mambo wasiyoyapenda, mambo ambayo hayana uhusiano na hulka zao. Watu wanafanya kazi lakini kwa lengo moja nalo ni kupata pesa pasipo kuwa na ridhaa katika nafsi zao. Kwa mujibu ya mwanasaikolojia Abraham maslow binadamu anasukumwa kukua na mambo mengi lakini kuu kuliko yote ni nafsi yake kuridhika.

Nafsi yako isiporidhika na kuridhia kazi unayofanya jua kabisa lazima utakosa msukumo na furaha katika kazi hiyo. Utaanza kuingiwa na hisia hasi kila unapokumbuka kwamba kesho yake kuna kazi. Steve Jobs aliwahi kusema kuwa kama hujapata kitu unachokipenda endelea kutafuta maana maana kuu ya maisha ni kutafuta kusudi lako na kulifanya.

Kama kwa mtazamo wa Dale carnegie inatupasa kujizamisha katika kazi tunayoiamini kwa mioyo yote na kuziishi kazi hizo utapata furaha na hautokaa kusubiri Jumatatu ifike uruke katika kazi ya moyo wako na uzuri ni kwamba ukiishi kazi ya moyo wako hautokuwa na likizo.

Friday, August 19, 2016

NJIA ZA KUDHIHIRISHA MAONO YAKO

"Whatever you vividly imagine, ardently desire, sincerely believe, and enthusiastically act upon must inevitably come to pass!" - Paul J. Meyer

Tafakari ya ufasaha ni ngazi ya kwanza kabisa ya kufikia unachokitaka. Mara nyingi huwa tunatafakari bila ufasaha. Tunabeba maono makubwa lakini hatukai chini kutafakari maono hayo kwa ufasaha. Ni muhimu kukaa chini kutafakari kwa ufasaha maono uliyonayo.

Hitaji kutoka ndani ya nafsi ni ngazi ya pili kwa mujibu wa paul meyer ya kufikia malengo. Lazima maono yako uyatengenezee sababu na msingi wa ndani wa kihisia. Tengeneza msukumo wa ndani wa uhitaji katika kufikia malengo yako...Lazima utengeneze sababu ya kwanini unatakiwa ufikie malengo hayo.

Amini kutoka moyoni ni ngazi ya tatu kwa mujibu wa Paul meyer, ni lazima uwe na imani thabiti juu ya maono yako na imani hiyo isitetereshwe na aina yeyote ya mazingira. Ukiwa na maono lakini ukashindwa kuyaamini maono yako jua hautoweza kuyafikia.

Kisha unatakiwa uchukue hatua kwa msisimko na mhemko chanya. Lazima uchukue hatua kwa msisimko na mhemko chanya la sivyo hutoweza kuyafanya hayo maono yako dhahiri. Hatua iliyo na msisimko itakuwezesha kushinda vipingamizi au misukumo na changamoto hasi.
Kwa mujibu wa Paul meyer chochote kitafanikiwa ukifata hizo njia.

Tuesday, August 16, 2016

JE UNA UHUSIANO NA UNACHOKIFANYA

Changamoto kubwa watu wengi wanayokutana nayo katika mambo wayafanyayo ni kukosa uhusiano wa kihisia baina yake na akifanyacho. Lazima kuwe na msingi na uhusiano wa kihisia na kinafsi baina yako wewe na unachokifanya.

Ukikosa huo uhusiano lazima ukose hisia ya kuridhia na kuridhika kwa kile ukifanyacho. Bado katika nafsi yako kunakuwa na utupu ambao husababisha hisia za upweke katika kila ukifanyacho. Kuna watu wengi wanafanya kazi au shughuli lakini wana upweke kwa yale wayafanyayo.

Nafsi yako inakosa uwiano na kile ukifanyacho. Uwezo wako unakosa msukumo kuelekea kile ukifanyacho. Ni changamoto kubwa pale unapotaka likizo ili upumzike kihisia ktk kile ukifanyacho maana kazi ya nafsi yako huwa haina likizo ya kihisia.

Ukiona msukumo wako unapungua na hauna ile shauku ya kuongeza msukumo kiutendaji katika jambo fulani ni dhahiri wewe na hilo jambo hamna uhusiano wa kimsingi wa kinafsi na kihisia. Lazima kuwe na uhusiano, tafuta jambo ambalo lina mahusiano na nafsi yako.

Wednesday, August 10, 2016

NANI MUANDAAJI WA SCRIPT YA MAISHA YAKO?

Ni utaratibu kwa waigizaji wa filamu kuandikiwa muongozo wa jinsi ya kucheza tamthilia au filamu kwa kuvaa uhusika wa watu walio katika nadharia. Wao huvaa uhusika na kucheza kwa muongozo wa mtayarishaji mkuu.

Katika maisha yako ni nani mtayarishaji mkuu wa script unazocheza? Kuna kipindi lazima uvae uhusika wa mtu fulani aliye katika nadharia nawe umuweke katika matendo lakini ni muhimu sana kutambua ni nani mtayarishaji mkuu wa script zako.

Mtayarishaji mkuu anaweza akawa Mzazi wako, ndugu zako na hata majirani zako inategemea na nani umempa funguo ya kukushurutisha, unapompa utayarishaji mkuu mtu mwingine unaishi katika maono au nadharia ya mtu mwingine. Naye ndo anakuwa mtengeneza utaratibu wa maisha yako. Ni sawa na mtumwa, yeye huishi akifata utaratibu wa Bwana wake.

Unapoacha kuwapa watu wengine utayarishaji mkuu wa script za maisha yako ndipo unapoanza kuishi maisha yako, ndipo unapoanza kuishi ndoto zako na maono yako, tofauti na hapo unakuwa mtumwa wa maono na nadharia za watu wengine.

Changamoto kubwa ni kutengeneza script ya maisha yako na usimame imara kama msimamizi mkuu kwa vitendo na usikilize mawazo yale yanayoendana na hiyo script yako na sio siri ni lazima utapata upinzani kutoka kwa wale ambao wanataka kuwa watayarishaji wa script ya maisha yako na mara nyingi ni watu wale ambao hata wao walitayarishiwa script za maisha yao wanataka kuendeleza utamaduni huo.

Andaa miongozo, andaa script na uhakikishe unajenga mianya ya watu watakaokuwezesha kucheza vizuri script yako, wawe ni marafiki, wakufunzi nk.
Kumbuka unaanza kuishi maisha yako pale unapokuwa mtayarishaji wa script ya maisha yako .