Monday, November 21, 2016

KIWANGO CHA MAANDALIZI YAKO KIKOJE?

Kuna dhana inayosema njia pekee ya kutabiri hatma yako ni kuitengeneza na ukishindwa kujiandaa unajiandaa kushindwa. Ni dhana zenye ukweli kabisa katika maisha yetu ya kila siku. Maandalizi ni jambo ambalo linaweza kukuonyesha hatma ya mchezo, yawezekana dhana hii isiwe na uhalisia wa jumla katika maeneo mengine hasa pale watu wanapojiandaa lakini bado wanashindwa. Jambo la muhimu ni je unajiandaa kwa kipimo gani na pia unajiandaa katika msingi upi.

Kutokujiandaa na kujiandaa kwa jambo lisilo na uwiano na hatma yako inaweza leta changamoto sawa jambo hilo linapofika. Kuna mambo yanaweza fika ukashindwa kuyahimili kwasababu hukuwa na maàndalizi imara kuyahimili hayo mambo.

Nataka nizungumzie juu ya maswali ambayo watu wanakuwa nayo hasa wanapokuwa wakisubiria jambo fulani litokee, mara nyingi hukaa wakitazama wengine ambao wanategemea jambo hilo hilo au lenye usawa wa namna hiyo wakisonga mbele na kulipata huku wao wakiendelea kusubiri, Maandalizi yanaweza kuwa ya muda mrefu au muda mfupi inategemea na uzito wa jambo lako.

Ukienda katika sehemu ya mgahawa ukaagiza chakula cha thamani sana au chakula kinachohitaji maandalizi utasubiri sana na pengine utashangaa mwingine anayekuja kuomba kinywaji akiandaliwa na kupata mapema, ukadhani labda unafanyiwa makusudi, hapana maandalizi ya chakula chako yanahitaji muda kwasababu umeomba chakula kinachohitaji umakini, muda na uwekezaji mkubwa kukiandaa, hivo haimaanishi kuwa umefanya makosa kuagiza chakula hicho.

Wengi wamejikuta wakibadilisha matazamio yao na kuamua kufanya mambo tofauti na matazamio yao kwasababu maandalizi yao yamekuwa ya muda mrefu. Tatizo halikuwa katika muda wa maandalizi bali tatizo lilikuwa katika uwezo wa kusubiri na misukumo ya kulitwaa jambo lile kwa wakati huo.

Cha msingi ni kuhakikisha unajiandaa katika kila jambo unalolihitaji, usiseme nitajiandaa hilo jambo likija, muda mwingine unaweza jiandaa lakini usifanikiwe kwa wakati huo, haimaanishi maandalizi yako hayakuwa na mantiki, hapana endelea na maandalizi. Katika maandalizi kuna tabia zinaimarika, kuna uwezo unajengeka ndani mwako ambao utakuwezesha kuwa na ufanisi katika hilo jambo litakapokuja.

Tambua kwamba maandalizi siku zote ni jambo endelevu, usichukie vipindi vya maandalizi na kila wakati jua unajiandaa kwa jambo fulani. Haijalishi maandalizi yako yanachukua muda gani. Usiupime muda wa maandalizi pima kiwango cha maandalizi yako. Maandalizi huongeza thamani yako na uwezo wako

2 comments: