Thursday, November 10, 2016

KUDHIBITI HISIA HASI

Magugu siku zote huota hata sehemu ambazo hazitakiwi, hayaitaji mbegu..yenyewe huota bila kupandwa wala nini, vivo hivo na hisia hasi, huwa haziitaji kazi kubwa kukaa katika nafsi yako. Zinaweza kukuhijia wakati wowote na kwa namna yeyote lakini hisia chanya zinahitaji kupangiliwa, kurutubishwa na kupaliliwa.

Moyo wako kuna wakati unaweza patwa na hisia hasi ambazo zinakuja kutokana na jambo lolote, inawezekana ni uchovu wa kimwili au kiakili, mtu fulani kukukatisha tamaa, mtu fulani kuzungumza na wewe vibaya nk...yamkini ni mtu wako wa karibu, au mtu ambaye ana mguso wa tofauti ndani ya moyo wako. Lakini ni vyema ukatengeneza mzani wa kupima hisia hasi na kuzikata badala ya kuzipa hifadhi kwa muda mrefu ndani yako.

Ukizipa hifadhi kwa muda mrefu zina tabia ya kuchoma nafsi yako na kila zikichoma nafsi yako zinakujengea hali ya kutaka kuzitoa. Na hapo wengi wamejikuta wakizitoa kwa msukumo unaosababisha maafa zaidi. Njia pekee ya kuzidhibiti hisia hasi ni kupumzisha nafsi yako kwa muda huku ukijaribu kuingiza hisia chanya.

Hisia chanya zinahitaji nidhamu kuziimarisha ndani ya nafsi yako, kwasababu asilimia kubwa ya watu wamezungukwa na mazingira hasi mfano ndugu walalamishi, marafiki wasiojali, wapendwa wasiokuelewa na wasioheshima uhuru wako na furaha yako. Inabidi ujipe likizo ya kinafsi. Ikiwezekana jijengee utaratibu hata wa kufunga kuendekeza hisia hasi kwa kipindi fulani kama jinsi ambavyo dini hufunga chakula au starehe fulani waweza funga kutoziendekeza hisia hasi.

Jenga utaratibu katika maisha yako wa kutozipa hifadhi hisia hasi wala kuziendekeza kwa muda mrefu. Hisia ni mfano wa mimea, kuna mimea bora na kuna magugu. Hisia hasi ni kama magugu. Tafuta kuwa mtu mwenye hisia chanya kila wakati. Ni sawa na chumba chenye uchafu na kila aina ya takataka...usipoweza kuondoa visivohitajika, chumba kitajaa na hewa itakuwa haizunguki vizuri. Usipoweza kupunguza hifadhi ya hisia hasi ndani ya nafsi yako, nafsi yako itajaa na hewa nzuri ya mazingira chanya haitozunguka vizuri ndani yako.


No comments:

Post a Comment