Monday, November 14, 2016

USITAFAKARI MAJUTO, TAFAKARI FUNDISHO

Katika maisha tunapitia mambo mengi, njia nyingi na tunakutana na vitu vingi, nafasi nyingi na hata vipindi vingi ambavyo tunatakiwa tufanye maamuzi juu ya mambo kadha wa kadha tunayokutana nayo. Kama binadamu wenye uhuru wa kufanya uchaguzi na utashi kila wakati huwa tunatumia njia zozote zile tulizonazo kufanya maamuzi.

Maamuzi yetu ndiyo ambayo hutengeneza hatima ya maisha yetu au matokeo yanayokuja baada ya hapo. Maamuzi mazuri huleta matokeo mazuri na maamuzi mabaya pia huleta matokeo mabaya. Kila mtu ameshapitia hali ya kufanya maamuzi na kila mtu ametumia uhuru wake wa kinafsi kufanya maamuzi. Changamoto kubwa ni matokeo ya maamuzi yetu na jinsi tunavopokea matokeo ya maamuzi yetu.

Maisha siku zote ni safari endelevu yenye changamoto mbali mbali na safari hiyo huwa vumilivu pale inapoendeka kwa maarifa na ujuzi wa wapi unaelekea. Maisha huhitaji dira na dira ndo itakuelekeza kasi ya kwenda nayo hata njia za kupita kufikia hatma yako. Maarifa ni muhimu sana.

Mara nyingi tumekuwa na mapokeo tofauti tofauti ya matokeo ya maamuzi yetu ambayo wengi wetu yametusababishia kukwama kwa muda mrefu katika dimbwi la maumivu na tukaishia kulalamika, kulaumu, kuwa na mitazamo hasi na hata kupata matatizo mbali mbali ya nafsi. Mara nyingi tumekuwa watu wa majuto badala ya mafunzo

Jambo la muhimu ni kutafakari mafunzo uliyoyapata na uyatumie hayo kama mawe ya kukanyagia kwenda mbele, usikae unajilaumu au unatafakari kwa makosa ya nyuma hata kama yameleta matokeo mabovu katika maisha, badala ya kusema ningejua tafakari aya sasa umejua utafanya nini. Huwezi kubadilisha makosa ya nyuma ila unaweza kufanya mabadiliko ili makosa ya nyuma yasijirudie.

Wengi tunakaa zaidi tunatafakari majuto badala ya kutafakari mafunzo na kufanya yanayohitajika kusonga mbele halafu baadaye unajikuta unarudia kosa lile lile au unapita tena njia ile ile. Badili mtazamo hata kama matokeo ya maamuzi yako mabaya yanaendelea kukutesa kuwa na ujasiri wa kusema nitafanya hivi badala ya ningefanya hivi.

Kumbuka kila mtu ameshafanya kosa fulani ambalo limemgharimu au linamgharimu hadi sasa lakini cha msingi ni kutafakari funzo badala ya majuto.

No comments:

Post a Comment