Monday, September 11, 2017

NAFASI YA MAZUNGUMZO YAKO KATIKA UTASHI WAKO WA KIHISIA

Je wajua kuwa mazungumzo yako ni kipimo cha utashi wako wa kihisia? Je wajua ya kwamba mazungumzo yako yana mchango katika uimara wa utashi wako wa kihisia. Jiulize tu swali moja, unazungumza nini?

Mfumo wako wa mazungumzo au uwasilishaji mawazo yako ni kipimo cha utashi wako wa kihisia. Jinsi unavozungumza juu ya maswala yenye miguso ya kihisia ndivo jinsi utashi wako wa kihisia ulivo. Watu wengi hudhani kuwa uhuru wa kuzungumza katika kutoa mitazamo ya kihisia ni sawa na uhuru wa kuzungumza katika maswala ya kiakili na kifikra, hapana. Uhuru wa kihisia unahitaji mguso wa kinafsi na ufahamu wa aina ya utu wa nafsi husika.

Watu wengi wamejikuta wanazungumza katika lugha hasi yenye harufu ya ukosefu wa imani na ladha ya uchungu wa maumivu kwakuwa ndivo utashi wao wa kihisia ulivo. Wengi wanazungumza nyuma ya pazia la woga na hofu wakionekana ni watu wenye uimara mkubwa kifikra kumbe kihisia ni nafsi ambazo zina hofu hata ya kupatwa na mawimbi ya kihisia. Ukiweza tambua miundo ya lugha na mitazamo utatambua kuwa kuna changamoto kubwa katika utashi wa kihisia.

Tambua ya kwamba kimjazacho mtu ndicho kimtokacho. Inatakiwa tutambue ni nini haswa hutujaza nafsi zetu. Kuna mazungumzo tunayopenda kuyapa nafasi pengine kwa utamu wake  wa kimaudhui wenye kuburudisha nafsi zenye shauku ya kutaka ufahamu pengine hata kama maudhui haina tija wala faida lakini mazungumzo hayo ndiyo yanajaza nafsi zetu magugu yanayoenda kusababisha udhaifu wa kihisia. Shauku isiyo na nidhamu ni adhabu kwa hisia na nafsi. Lazima ujifunze kuratibu mazumgumzo.

Kuna mazungumzo pia tunayofanya ambayo hutudhoofisha nafsi zetu na kutupa misukosuko ya kihisia isiyo na tija. Hivo ni muhimu kutambua na kufahamu aina ya mazungumzo na mguso wake kwa hisia zako

Hatuwezi kuwa watu wenye nafsi imara na utashi wa kihisia bila kuwa watu wenye kuratibu aina ya mazungumzo tunayofanya. Ni jambo gumu sana kuwa mtu mwenye mazungumzo yasiyo na tija kuwa na utashi wa kihisia pengine ni rahisi hata ngamia kupenya katika tundu la sindano. Lazima uwe makini na mazungumzo yako.

Ratibu vyema mazungumzo yako ili safari yako ya utashi wa kihisia iweze kuimarika.

No comments:

Post a Comment