Je wajua kila jambo bora huja na gharama ya uvumilivu. Kila jambo unalohitaji katika maisha huja na gharama ya uvumilivu huku ukikua katika nidhamu katika hicho kipindi cha uvumilivu. Kuna wakati unaweza dhani unaishi katika ndoto pale unapozungumza mambo pasipo kuyaona katika uhalisia.
Imani ni kuwa na uhakika wa mambo ambayo unayo katika fikra lakini bado hayajadhiirika. Unaweza omba msitu lakini ukapata mbegu ya msitu na ukaanza kujiuliza hii mbegu naifanyia nini. Unaweza kuwa na maono ya kujenga familia bora yenye kila hitaji muhimu likiwa limekamilika lakini ukajikuta unapata mwenza ambaye amekamilika katika hitaji la kinafsi lakini mahitaji ya kimali bado inakubidi uvumilie pengine hata uwekeze muda zaidi. Ni wewe kutambua kuwa hiyo uliyonayo ni mbegu bora inayohitaji udongo mzuri ili ichipue yale unayohitaji.
Hitaji la nafsi ni changamoto kubwa na wengi wamekuwa wakipata mahitaji mengine lakini wamekuwa wakiishi pasipo kuridhika kwakuwa mahitaji ya kinafsi wamekuwa wakiyakosa. Tambua kuwa kuna nyakati ambazo uvumilivu na imani yako itawekwa katika kipimo ili kuimarika katika uthabiti wa kimaamuzi. Kila jambo huwa zuri kwa muda kama likijengwa juu ya uaminifu, maono na nia thabiti ya kulisababisha lile jambo litokee katika uhalisia wake.
Lazima ufike kipindi ambacho imani yako itakuwa katika kipimo, lazima ifike kipindi utajiuliza je haya mambo ninayoyatazamia ni ndoto tu za mchana au kweli nitakuja kuyathibitisha. Unapofika katika kipindi hicho uimara wako na imani yako na fikra chanya ndizo zitakazokuvusha kuyapata yale unayoyahitaji na kuyatazamia.
Hakuna ndoto kwa mtu mwenye dhamira ya dhati na kila wakati anahangaika kutafuta njia za kutekeleza yale anayoyaona katika maono yake. Bali ni hatma ya muda na uvumilivu wa huyu mtu akisimama imara katika kutegemea yaliyo bora na yale anayoyatazamia. Usijione kuwa mwenye ndoto tu pengine labda unatazamia mambo ambayo kwa sasa huwezi yapata. Tambua kuwa dhamira ya dhati na utayari wa kujitoa huku ukichanganya na uvumilivu ukiendelea kukua kinafsi vitathibitisha ndoto zako na maono yako.