Wednesday, September 27, 2017
FREEDOM OF THE SOUL
Thursday, May 25, 2017
KUTOKA KATIKA UCHOVU WA KINAFSI
Uchovu wa kinafsi ni hali ya nafsi ya mtu kukosa nguvu ya kusimama ili kuweza kuhimili mitikisiko hasi. Ni hali ambayo kama ikiingia humjenga mtu kutaka ukombozi wa kinafsi na pumziko.
Kila uchovu unahitaji pumziko lakini njia za kupata pumziko ina utofauti. Kuna pumziko la kudumu na lile lisilo la kudumu. Watu wengi wamekuwa wakishindwa kutofautisha mapumziko hayo kutokana na kukosa taswira hada hasa pale uchovu unapokuwa mkubwa.
Changamoto kubwa ni uchaguzi wa pumziko la nafsi yako maana waweza fanya uchaguzi wa kudumu au wa muda mfupi ambao utakupa uchovu mkuu baada ya ganzi ya pumziko hilo kuisha.
Ili uweze kuchagua pumziko la kudumu ni lazima ujue chanzo kikuu cha uchovu wako wa kinafsi maana vichocheo vya uchovu huo mara nyingi ni kama mchwa ambao hukula taratibu nguvu yako ya kinafsi na kukuacha mchovu.
Unaweza pata uchovu wa kinafsi pale unapojaribu jambo linashindikana au pale unapotaka kubadili jambo inashindikana, unapotaka kubadili hali fulani lakini inashindikana au inaweza ikawa jambo fulani linakushambulia kila wakati ambalo unajaribu kuliepuka, au yawezakana ni watu ndo wanakupa uchovu wa kinafsi pale wanapoila amani yako, wanaposhambulia nguvu yako ya kusimama, na kutenda yale yanayovuruga misingi yako. Unaweza pata uchovu wa kinafsi na pengine ukajaribu kupata pumziko lakini ukashindwa katika uchaguzi wako ni lipi pumziko hasa unalohitaji.
Ukishindwa kujua hasa ni pumziko gani unalohitaji waweza jikuta unapata pumziko la muda mfupi ambalo likawa kama kilevi cha nafsi kisichokupa suluhisho la kinafsi la kudumu bali kinakupa nafuu ya muda mfupi tu.
Ukitaka kuondoa uchovu wa kinafsi siku zote jaribu kujitia nguvu kwa kuelekea zaidi pale ambapo panakutia nguvu, panakupa amani, panakupa mguso chanya, pana uwiano na kile unachokiamini, na pana misingi ya kiutu yenye uhusiano na nafsi yako.
Uchovu wa kinafsi humkuta kila mtu kwa wakati fulani lakini tofauti inakuja katika uchaguzi wa mapumziko. Waweza jikuta unajiingiza katika pumziko la muda mfupi ambalo badala ya kuitia nguvu nafsi yako linazidi kukudhoofisha.
Chagua vyema pumziko la nafsi yako ili uweze kuushinda uchovu wa kinafsi.
Monday, May 15, 2017
CHUNGA MOYO WAKO
Chunga moyo wako maana hiyo ndiyo bustani ya amani na furaha yako. Nafsi yako hustawi katika bustani ya moyo wako. Katika bustani ya moyo wako kunaweza kuwa na maua ya furaha, amani na faraja au magugu ya maumivu na uchungu. Kuwa muangalifu sana kwa kuchunga moyo wako kila wakati ni nini kinachoota.
Kuna mawazo na maneno ambayo ukiyaruhusu yaingie moyoni yanaenda kuweka majeraha ambayo kupona kwake kutakuchukua muda sana. Majeraha hayo yatajenga mfumo wa kifikra wa kujihami ili kuzuia maumivu mengine. Hasara ya fikra za kujihami ni kwamba utashindwa kufurahia uhuru na uzuri wa maisha kwa kuwa utaishi kwa kujihami.
Moyo wako unatakiwa ulindwe kama ngome imara. Ukiruhusu maumivu au matatizo yakaingia katika bustani ya moyo wako yataenda kuotesha magugu ya mawazo na fikra hasi. Kuna maneno ukiyaruhusu kuingia siku moja yatautesa moyo wako wakati wote.
Safisha moyo wako kwa kuondoa yale ambayo yanauumiza na kutesa moyo wako. Yale ambayo kila ukiyafikiria unasikia kama kichomi ndani ya moyo wako, yale ambayo kila ukiyapa nafasi katika akili yanakububujisha machozi ya uchungu moyoni mwako.
Tambua kuwa moyo wako unatakiwa kustawisha amani, furaha na upendo. Ukiwa na moyo wenye uchungu inageuka kuwa sumu inayodhoofisha nafsi yako na akili yako. Utakuwa mtu mwenye vifungo badala ya uhuru.
Chunga moyo wako na uache katika amani. Usiuache umekaa katika dimbwi la maumivu au usiuache ushikilie uchungu unaokuumiza, usiuache ushikilie maneno makali au misumari ya mitazamo hasi juu yako. Usiruhusu moyo wako udunde kwa kasi kwa kukosa amani au kuwa na taharuki, Jipe utulivu kwa kuruhusu uzuri na furaha istawishe moyo wako.
Ruhusu yale yenye furaha na amani na yenye uzuri na utulivu ndio yakae katika moyo wako. Stawisha moyo wako ili ukutunze na uachilie yale yenye furaha, amani na pumziko. Kama vile damu inavoingia na kutoka katika mkondo wa mishipa ya damu, wewe pia tengeneza mkondo wa kuingiza furaha nyingi, amani nyingi na faraja nyingi moyoni mwako kwa kukaa na watu au mazingira yatakayosaidia hivo vitu lakini ondoa moyoni mkondo wa maumivu, uchungu na yale yanayoutatiza moyo
Lazima kuwe na uwiano baina ya yanayotoka na yanayoingia, usipende kuingiza mawazo hasi, Itafute hiyo furaha na amani ili ustawishe bustani ya moyo wako.
Fikra chanya au mazingira chanya sio tu yale yanayokusukuma kufanikiwa bali pia kuustawisha moyo wako na kuuacha katika hali ya utulivu.
Tuesday, May 2, 2017
USICHUKULIE KILA JAMBO KIHISIA
Ukitaka kuwa na furaha usipende kuchukulia kila jambo kinafsi au kihisia. Kuna mambo mengine ni ya kifikra tu na yamekaa kimtazamo tu ambayo hayatakiwi kuchukuliwa kihisia.
Ukitaka kuwa na utashi wa kihisia na uweze kuratibu hisia zako katika mlengwa chanya yakupasa kuziacha hisia zako katika mfumo tulivo kadri uwezavyo. Kuna mambo ukiyachukulia kihisia utaziweka hisia zako kwenye mfumo wa taharuki kwa wakati mwingi na itakupunguzia msisimko wa maisha ulio katika muundo chanya.
Je wawezaje kutochukulia mambo kihisia? Tambua kuwa kila wazo au mtazamo unapaswa kupokelewa kiakili na kuratibiwa kabla ya kusukumwa na hisia fulani. Ni vizuri ukiratibu mawazo na mitazamo unayopokea na kuiratibu kabla ya kujua ni hisia gani uiachilie ili isukume hilo jambo.
Ni muhimu sana kulishikilia wazo au mtazamo katika mfumo chanya hata kama limekuja katika muundo hasi. Lione hilo wazo kama njia ya kukuboresha, yaone hayo maoni kama njia ya kukuboresha kisha yape hisia chanya ndipo uyapokee. Usikubali kuanza kupokea kihisia wazo ambalo hujariratibu kwa akili.
Mfano mtu anaweza kukwambia jambo ambalo unaona kabisa linaweza lisiwe chanya kwako, badala ya kulipokea kwa hisia hasi jaribu kuliona ilo jambo kama wazo la kukuboresha na sio kukuharibu, kisha chukua hisia ya amani na furaha kwa kutambua kuwa hilo wazo limekuja kukuboresha..kisha chukua hisia ya morali na ari ya kulitafutia ufumbuzi na kulishughulikia hilo jambo na sio vinginevyo. Ukilipokea kama vile limekuja kukuumiza utaingiwa na taharuki ya kinafsi pengine hata kujenga ukuta kulizuia hilo suala na kuonekana kuwa ni mtu dhaifu kinafsi pengine hata mtu hasiyependa kuambiwa ukweli.
Nakushauri tena usilipokee kila jambo kihisia kabla ya kuriratibu kiutashi na kiakili ili kukujenga utashi wa kihisia itakayokupa furaha wakati wote.
Sunday, April 23, 2017
TAFUTA AMANI YA NAFSI
Hakuna jambo lenye msingi katika uimara na utashi wa nafsi kama amani ya nafsi - Nickvaleries
Huwezi kukua katika utashi wa nafsi pasipo kuwa na amani ya nafsi. Imani ikikaa katika nafsi humuwezesha mtu kustahimili misukosuko ya nje kwasababu kinachoweza kuzamisha meli sio bahari bali maji yanayoingia ndani ya meli.
Ukiweza kuiacha nafsi yako katika usalama kwa kujenga ukuta kuzuia yale yanayotokea yasiondoe amani ya nafsi utaweza kustahimili mengi. Ukikosa amani lazima utakosa imani na ukikosa imani hata utendaji wako na maneno yako yatakwenda kinyume na uhalisia.
Jiulize ni mambo gani ambayo unayaruhusu katika nafsi yako...Je yanaimarisha ngome za utulivu wako au yanabomoa amani ya nafsi yako na kukupa hali ya taharuki. Waweza kuwa na vyote ukakosa amani na ukikosa amani ukakosa imani huweza kuwa na furaha.
Hakuna furaha mahali palipokosa amani...Huwezi kuwa na furaha ya nafsi au kufurahia yale mazuri yanayokuzunguka kama ukikosa amani. Tafuta kuwa na amani na jiimarishe kinafsi ukiziimarisha ngome za nafsi yako.
Jitahidi kujenga ngome zenye usalama ndani yako kiasi cha kusimama imara kinafsi hata kama mazingira ni yenye taharuki..sikiliza ulimwengu una taharuki na ukikosa amani jua huwezi kuwa na furaha.
Amani inaweza patikana kwa kuimarisha misingi ya uaminifu, mawasiliano, utashi wakihisia na utu. Tambua kwamba kila jambo linafanyika kuwa jema na wewe ni mwenye hatma njema na kuna mambo mengi mazuri ambayo yako mbele yako.
Taswira yako ni ya muhimu sana ukitaka kuwa na amani. Je unaangalia nini na unasikiliza nini? Hakikisha umejiimarisha kuratibu kila kinachoingia katika nafsi yako.
Usipende kuyapa muda mwingi mawazo na mazingira yanayoondoa amani yako. Itenge nafsi yako ili iwe na amani.
Tuesday, March 28, 2017
JENGA UTASHI WA KIHISIA
Uimara wa mtu katika nafsi umejikita zaidi katika utashi wake wa kihisia. Binadamu ni kiumbe chenye nafsi na nafsi ya mtu imeundwa katika mfumo wa hisia. Hisia za mtu pia zimeundwa katika mfumo wa utu wake. Kila mtu ana muundo wake wa kiutu ambao ndio msingi hasa wa uratibu wa hisia za mtu huyo.
Hisia ni misukumo na mihemko ya kinafsi ambayo hujitokeza kutoka kipindi hadi kipindi kutokana na mabadiliko ya ndani au nje. Yaweza ikawa mabadiliko ya kimazingira au mabadiliko ya tabia za mwili. Changamoto kubwa ya hisia ni kwamba ni kama upepo, huja na kufika katika kilele lakini baadaye hushuka katika ukawaida na pengine hushuka zaidi ya hapo.
Hapo ndipo wengi hujikuta wanasema leo najihisi niko chini sana kihisia au nimezama katika hisia na hata wengi hutumia kauli za vitabu vya dini na kusema leo nimezama katika bonde la uvuli wa mauti. Lakini hao hao watu nyakati nyingine utasikia anasema leo nina msisimko au leo niko hewani. Yote hayo ni mabadiliko ya kihisia.
Hisia zinaweza kuwa nzuri kama zikitumika vizuri lakini changamoto kubwa ni pale mfumo wa uratibu wa kimaamuzi katika akili unapofungwa katika hisia ambazo zinapanda na kushuka. Kuna ambao wamekuwa na utashi wakufikiria lakini wamekosa utashi wa kihisia.
Utashi wa kihisia ni uwezo wa kuratibu hisia zako na kuzielekeza vile unavotaka. Watu wengi tumekuwa na utashi wa ki akili lakini tumekosa jambo la muhimu sana ambalo ni utashi wa kihisia kupelekea yale tunayoyajenga kwa akili zetu yanaharibiwa na hisia zetu.
Waweza fikiria jambo zuri na ukaliwekea mikakati madhubuti lakini kinapofika kipindi cha mtikisiko unaogusa hisia ,wengi wetu tumejikuta tukiruhusu hisia zetu ziharibu hata ule mtazamo chanya wa yale tuliyoyajenga kwa akili zetu.
Watu wengi waliofanikiwa au wakuu wamejikuta wakianguka na kufanya maamuzi mabovu kwasababu ya kukosa utashi wa kihisia na wamejikuta wakizama katika dimbwi ambalo pengine kusababisha zile imaya walizozijenga kwa akili nyingi kuanguka kutokana na kukosa utashi wa kihisia.
Wekeza sana kuwa utashi wa kihisia uweze kutambua ni hisia zipi zinakujenga na zipi zinakubomoa. Hisia zipi zinakuimarisha na hisia zipi zinakudhoofisha, hisia zipi zinakuinua na hisia zipi zinakuangusha. Ukiwa na utashi wa namna hiyo utaweza kuzitumia hisia hizo ziweze kukutumikia na sio wewe kutumikia hisia zako.
Je wawezaje kuwa na Utashi wa kihisia
1. Pambanua hisia zako pindi zinapokuja na utambua mlengwa wa kila hisia.
2. Tambua chanzo cha hisia husika au mifumo sababishi ya kutokea kwa hisia hizo.
3. Jifunze kuzimudu hisia kila zinapokuja kwa kuifanya nafsi yako izungumze na hisia hizo
4. Tambua kuwa hisia sio jambo baya na wala sio udhaifu bali ni muundo wa kinafsi hivo hisia zako zikubali kuwa ni zako na wewe ndio mwenye kuwajibika kwa hisia hizo. Usitafute kisingizio juu ya hisia zako.
5. Jiimarishe katika uvumilivu ili uweze kuziratibu hisia zako na kuratibu mkondo wa hisia zako maana hisia ni kama mkondo wa maji
6. Pendelea kutenga muda wako wa upekee ukizungumza na nafsi yako ili uweze kuthibitika katika uimara wa kihisia.
Hakuna jambo la msingi na lenye kufaa kama kuwa na utashi wa kihisia maana maisha yako yanaweza kuwa yenye furaha na amani au kuwa na shida na maumivu kama hauna utashi wa kihisia.
Monday, January 16, 2017
GHARAMA NA KIPIMO CHA UVUMILIVU
Je wajua kila jambo bora huja na gharama ya uvumilivu. Kila jambo unalohitaji katika maisha huja na gharama ya uvumilivu huku ukikua katika nidhamu katika hicho kipindi cha uvumilivu. Kuna wakati unaweza dhani unaishi katika ndoto pale unapozungumza mambo pasipo kuyaona katika uhalisia.
Imani ni kuwa na uhakika wa mambo ambayo unayo katika fikra lakini bado hayajadhiirika. Unaweza omba msitu lakini ukapata mbegu ya msitu na ukaanza kujiuliza hii mbegu naifanyia nini. Unaweza kuwa na maono ya kujenga familia bora yenye kila hitaji muhimu likiwa limekamilika lakini ukajikuta unapata mwenza ambaye amekamilika katika hitaji la kinafsi lakini mahitaji ya kimali bado inakubidi uvumilie pengine hata uwekeze muda zaidi. Ni wewe kutambua kuwa hiyo uliyonayo ni mbegu bora inayohitaji udongo mzuri ili ichipue yale unayohitaji.
Hitaji la nafsi ni changamoto kubwa na wengi wamekuwa wakipata mahitaji mengine lakini wamekuwa wakiishi pasipo kuridhika kwakuwa mahitaji ya kinafsi wamekuwa wakiyakosa. Tambua kuwa kuna nyakati ambazo uvumilivu na imani yako itawekwa katika kipimo ili kuimarika katika uthabiti wa kimaamuzi. Kila jambo huwa zuri kwa muda kama likijengwa juu ya uaminifu, maono na nia thabiti ya kulisababisha lile jambo litokee katika uhalisia wake.
Lazima ufike kipindi ambacho imani yako itakuwa katika kipimo, lazima ifike kipindi utajiuliza je haya mambo ninayoyatazamia ni ndoto tu za mchana au kweli nitakuja kuyathibitisha. Unapofika katika kipindi hicho uimara wako na imani yako na fikra chanya ndizo zitakazokuvusha kuyapata yale unayoyahitaji na kuyatazamia.
Hakuna ndoto kwa mtu mwenye dhamira ya dhati na kila wakati anahangaika kutafuta njia za kutekeleza yale anayoyaona katika maono yake. Bali ni hatma ya muda na uvumilivu wa huyu mtu akisimama imara katika kutegemea yaliyo bora na yale anayoyatazamia. Usijione kuwa mwenye ndoto tu pengine labda unatazamia mambo ambayo kwa sasa huwezi yapata. Tambua kuwa dhamira ya dhati na utayari wa kujitoa huku ukichanganya na uvumilivu ukiendelea kukua kinafsi vitathibitisha ndoto zako na maono yako.
Thursday, November 10, 2016
KUDHIBITI HISIA HASI
Magugu siku zote huota hata sehemu ambazo hazitakiwi, hayaitaji mbegu..yenyewe huota bila kupandwa wala nini, vivo hivo na hisia hasi, huwa haziitaji kazi kubwa kukaa katika nafsi yako. Zinaweza kukuhijia wakati wowote na kwa namna yeyote lakini hisia chanya zinahitaji kupangiliwa, kurutubishwa na kupaliliwa.
Moyo wako kuna wakati unaweza patwa na hisia hasi ambazo zinakuja kutokana na jambo lolote, inawezekana ni uchovu wa kimwili au kiakili, mtu fulani kukukatisha tamaa, mtu fulani kuzungumza na wewe vibaya nk...yamkini ni mtu wako wa karibu, au mtu ambaye ana mguso wa tofauti ndani ya moyo wako. Lakini ni vyema ukatengeneza mzani wa kupima hisia hasi na kuzikata badala ya kuzipa hifadhi kwa muda mrefu ndani yako.
Ukizipa hifadhi kwa muda mrefu zina tabia ya kuchoma nafsi yako na kila zikichoma nafsi yako zinakujengea hali ya kutaka kuzitoa. Na hapo wengi wamejikuta wakizitoa kwa msukumo unaosababisha maafa zaidi. Njia pekee ya kuzidhibiti hisia hasi ni kupumzisha nafsi yako kwa muda huku ukijaribu kuingiza hisia chanya.
Hisia chanya zinahitaji nidhamu kuziimarisha ndani ya nafsi yako, kwasababu asilimia kubwa ya watu wamezungukwa na mazingira hasi mfano ndugu walalamishi, marafiki wasiojali, wapendwa wasiokuelewa na wasioheshima uhuru wako na furaha yako. Inabidi ujipe likizo ya kinafsi. Ikiwezekana jijengee utaratibu hata wa kufunga kuendekeza hisia hasi kwa kipindi fulani kama jinsi ambavyo dini hufunga chakula au starehe fulani waweza funga kutoziendekeza hisia hasi.
Jenga utaratibu katika maisha yako wa kutozipa hifadhi hisia hasi wala kuziendekeza kwa muda mrefu. Hisia ni mfano wa mimea, kuna mimea bora na kuna magugu. Hisia hasi ni kama magugu. Tafuta kuwa mtu mwenye hisia chanya kila wakati. Ni sawa na chumba chenye uchafu na kila aina ya takataka...usipoweza kuondoa visivohitajika, chumba kitajaa na hewa itakuwa haizunguki vizuri. Usipoweza kupunguza hifadhi ya hisia hasi ndani ya nafsi yako, nafsi yako itajaa na hewa nzuri ya mazingira chanya haitozunguka vizuri ndani yako.
Thursday, October 13, 2016
SAUTI TATU KATIKA MAHUSIANO
Mahusiano yetu huguswa na sauti ambazo zinaleta changamoto na ni sauti ambazo zinamchango katika uimara wa mahusiano yako au kuanguka kwa mahusiano yako. Bila sauti hizo kuwa katika uwiano sawa basi sauti moja ikiizidi nyenzake inaweza sababisha changamoto.
Sauti hizo zimegawanyika katika makundi matatu, ya kwanza ni sauti ya nafsi ; Hii ni sauti ambayo kila mtu anakuwa nayo kiasili nayo ni sauti ya uhuru, furaha na amani. Kila nafsi inataka kuwa katika uhusiano ambapo itakuwa huru na yenye furaha na amani, sauti hii inalia kutoka ndani ya nafsi ya mtu na ndio maana kuna ambao husema kuwa katika uhusiano ambao utakuwa huru na mwenye furaha na amani.
Sauti ya pili ni sauti ya Jamii; hii ni sauti inayotoka katika jamii inayotuzunguka juu ya mahusiano yetu. Hii sauti inaweza ikawa sauti ya wazazi au sauti ya malezi na makuzi ambayo tumeyapitia. Sauti hii mara nyingi hutuambia kuwa ni nani anatufaa, au ni nani tunatakiwa tuwe naye au ni mahusiano gani ambayo inabidi tuwe nayo.
Sauti ya tatu ni sauti ya akili zetu; Binadamu huwa na hali ya kupenda kutafakari na kutumia akili katika kufanya maamuzi na pengine kuna wakati hutumia zaidi akili katika mambo fulani juu ya nini hasa jambo sahihi la kufanya.
Ili kujenga uhusiano imara lazima hizi sauti ziwe na uwiano...sauti ya nafsi inabidi iwe kama msingi itakayobeba sauti nyingine zote. Sauti ya nafsi ikizifunika sauti nyingine zote unaweza pelekea kufanya mambo ambayo yanaweza kutokubalika katika jamii na ukajikuta unakosa kabisa ushirikiano na wengine lakini sauti ya jamii ikiizidi sauti ya nafsi utajikuta unaingia katika mahusiano ambayo katika jamii unasifika lakini ndani ya nafsi yako unakosa furaha na unakuwa na upweke ambao jamii haiwezi kukusaidia.
Pia inakupasa sauti ya nafsi iwe na uwiano na sauti ya akili ili akili yako iweze kuwekeza zaidi...maana nafsi na akili zikiwa na uwiano ile amani na furaha hudhiirika katika fikra za ubunifu zaidi katika kuimarisha mahusiano hayo.
Kama unaona sauti ya jamii ni kubwa na inakutisha hakikisha sauti ya nafsi na sauti ya akili vinaungana kuishurutisha sauti ya jamii itulie.
Changamoto na jambo la msingi kwa kila mtu ni kuhakikisha hizo sauti zina uwiano ili kujenga mahusiano imara.
Saturday, October 1, 2016
USIOGOPE KUKUTANA NA HOFU YAKO
Thursday, September 22, 2016
UHURU NA UDHIBITI WA KIHISIA
Uhuru wa kihisia ni pale unapoweza kudhibiti na kuelekeza hisia zako katika muundo na mpangilio uutakao. Hili si jambo rahisi kwa maana hisia huja kutokana na mabadiliko ya ndani ya mwili na hata hujengeka katika msingi wa nafsi ya mtu hivo uhuru wa kihisia unawezekana pale tu unapojenga tabia inayoitwa Nidhamu.
Nidhamu itakuwezesha kudhibiti hisia zako kwa namna kwamba utaweza kuzielekeza au kuamua muitikio na hata namna ya kukabili hali fulani zinazojitokeza. Uhuru wa kihisia kwanza unajengwa na kuitambua nafsi yako....nguvu na mapungufu yake kisha kujenga msingi wa kimaamuzi unaotokana na sheria utakazozijenga katika akili yako.
Hisia ni kama upepo, huja na hupoa na pengine hata kupotea kabisa, upepo huo unaweza kuwa kimbunga kwako au unaweza kuwa kama kipupwe kutokana na misingi ya kinidhamu ulioijenga katika nafsi yako ambayo inakupa uhuru wa kuamua jinsi hisia zako zinavodhibitiwa. Kudhibiti hisia ni sawa na kujenga mifereji ili kudhibiti mikondo ya maji isilete madhara au isielekee kusikotakiwa.
Ukiwa mfungwa wa hisia inamaana utendaji wako au muitikio wako katika mambo utatokana na msukumo wa hisia ulizonazo. Umeshawahi kuwa hisia nzito juu ya mtu fulani au jambo fulani kwa wakati fulani na ukatamani kulifuatilia lakini baada ya muda unapoteza hiyo hisia? Na hii hasa ndio changamoto ya kufanya maamuzi kwa kufuata hisia.
Jenga utaratibu wa kinidhamu wa kuratibu hisia zako kisha zielekeze kuongeza msukumo ktk sheria ulizozijenga na wala usiruhusu hisia zako zikuelekeze kupingana na sheria zako...namaanisha usiruhusu hisia pinzani zipate nguvu. Hisia zote zielekeze unapotaka ziende. Na hii inahitaji mazoezi.
Warren buffet aliwahi kusema kuwa mtu asiyeweza kudhibiti hisia zake hawezi kudhibiti pesa zake. Na hilo ni jambo la kweli kabisa, usipoweza kuwa nidhamu ya kihisia huwezi kuwe na nidhamu ya kiuchumi
Pia usipokuwa na uhuru wa kihisia utakuwa mhanga wa maumivu mengi ikiwemo mahusiano au hata namna watu wanavoleta upinzani katika maisha yako. Watu wasio na uhuru wa kihisia mara nyingi hushindwa kuchanganua ni aina gani ya mahusiano ni mazuri kwao na yatakayowajenga, kwao hisia zikishatawala wanashindwa hata kuruhusu akili zao kuchanganua.
Maisha bila uhuru wa kihisia ni kama msitu maana kila aina ya mabadiliko yatakuwa na mguso kwako na utataka kuitikia kila ambavyo hisia zitakutuma. Lazima uwe huru kuzidhibiti hisia la sivyo zitakuzamisha.