Kila binadamu ana uhalisia wake na utofauti wake, binadamu wanaweza fanana tabia lakini kuna msingi wa ndani kabisa wa kinafsi unaowatofautisha. Huu msingi wa kinafsi ndio uhalisia wa yule mtu. Mtu yeyote anayetoka katika uhalisia wake anapoteza utambulisho wake na akipoteza utambulisho wake anapoteza mambo mengi ya kinafsi yaliyomo ndani yake maana inambidi atafute uhalisia mwingine na alazimike kuishi katika uhalisia huo.
Kuna mambo mengi ya kinafsi ambayo mtu hupoteza na kuu kuliko yote ni amani ya nafsi na furaha ya ndani. Hapo ndipo unakutana na mtu ana kila kitu lakini hana furaha wala amani, yamkini kuna mambo kadha wa kadha yanayomtatiza lakini kuu kuliko yote ni kupoteza uhalisia wake. Kuna mambo yanayompa mtu ujasiri wa ndani, kuna misingi ya kinafsi ambayo mtu anakuwa nayo inayompambanua. Akipoteza hivo vitu au akitoka nje ya hivo vitu utaona mabadiliko yake kimtazamo na hata kihisia.
Katika uratibu wa kihisia na kutengeneza uimara wa kihisia mtu lazima arudi katikà uhalisia wake. Watu wengi wamepoteza dira katika mambo mengi kwasababu walitoka katika uhalisia wao ndipo wanakuja kushtuka wameshapotea na wakajikuta wanaishi kama wahanga wa mambo pasipo kujua nini cha kufanya.
Jitambue na jitambulishe na jiimarishe katika uhalisia wako maana utakapokuja kutoka katika uhalisia huo utajaribu kuwa kitu au mtu ambaye haumuelewi hata wewe. Unakuwa kama mtu usiyejitambua, Rudi katika uhalisia wako ili urudishe ile morali na msukumo na msisimko wa ndani kufanya mambo.
Ukiwa katika uhalisia wako mazingira ndo yatalazimika kuendana na uhalisia wako lakini tofauti na hapo wewe ndo utalazimika kuendana na mazingira. Uhalisia hukupa wewe uhuru wa kujipambanua na kujiwasilisha katika jamii ili uwe na mguso chanya. Uhalisia wako ndio hupelekea wewe kutambua kusudi lako na hata kuongeza thamani yako ili ulitende kusudi lako. Hivo ni muhimu sana kuwa katika uhalisia wako.
Jamii au mazingira yasikufanye upoteze uhalisia wako. Jamii ndo inapaswa ipishe njia ili uhalisia wako uweze kuwa na mguso na hii itawezekana tu ukisimama katika kulinda uhalisia wako
No comments:
Post a Comment