Saturday, March 25, 2017

MUDA WAKO WA UPEKEE NA NAFSI YAKO

Ukitaka kuwa na furaha anza kwa kufurahia muda wako wa upekee.

Moja ya changamoto tulizonazo kama binadamu ni upweke. Upweke sio ukosefu wa wenza au watu wa kutuzunguka. Upweke ni pale mtu anaposhindwa kuufurahia upekee wake na anaposhindwa kuwa na uhusiano na uhalisia wa nafsi yake.

Kuna malalamiko mengi unasikia hata katika mahusiano mmoja wao anasema nilijihisi mpweke ndo maana nilikusaliti, au mwingine anaingia katika ulevi au hata mikanda ya ngono kwa sababu ya upweke. Tafsiri yetu ya upweke ni kukosa watu wa kutengeneza muungano wa kinafsi au watu wa kuburudisha nafsi zetu.

Nafsi ya binadamu kila wakati inahitaji kurutubishwa kwa kutengewa muda wa kupata uwepo. Nafsi yako ni utu wako wa ndani. Mtu wako wa ndani anahitaji wewe umtengee muda kumsikiliza, kumdadisi, kuzungumza naye, kumburudisha na hata kumponya na aina yeyote ya maumivu.

Lazima ujitengee muda wako wako bora wa kutengeneza mguso wa kimaelewano na nafsi yako. Watu wengi wameshindwa kuwa watu wa namna hiyo kupelekea kupigwa na upweke kila wakati anapokosa mguso wa nje wa watu wanaomzunguka.

Rafiki yako wa kwanza na wa karibu ni nafsi yako. Itengee muda nafsi yako ili ipate ukaribu wako. Na wakati wa kuzungumza na nafsi yako jua kwamba unaongea na mtu wako wa karibu. Acha kuongea na nafsi yako kwa ukali au kuihukumu kwa makosa ya nyuma. Itie moyo nafsi yako, ikumbushe uwezo wako. Panda mbegu chanya ndani ya nafsi yako, itie moyo, iponye kwa makosa ya nyuma na iahidi mambo mazuri huko mbele, iburudishe kwa lugha nzuri yenye mguso chanya lakini kuu kuliko yote iweke huru.

Watu wengi wamekuwa wakitumia wakati wao wa upekee kwa kulala, kuangalia mitandao ya kijamii au hata kutafuta magenge ya umbea kutafuta jambo la kufanya kuondoa upweke nk. Huo sio wakati wake. Huo ni wakati wa kujenga uhusiano na nafsi yako. Ni sawa na aina yeyote ya uhusiano. Lakini uhusiano wako na nafsi ndiyo jambo la msingi kwanza.

Ukiwa na tabia ya kuwa na muda mwingi na nafsi yako hautokuwa mtu wa kulalamika upweke. Na hautokuwa mtu wa kutafuta vileta msisimko vya nje kama pombe, anasa na ngono pale unapojihisi mpweke. Utaufurahia muda wako wa upekee, nafsi yako itarutubishwa na utakuwa ni mtu mwenye furaha muda mwingi.

Angalizo ni kwamba katika muda wako wa upekee na nafsi yako hakikisha unatengeneza mazingira chanya. Huwezi kutengeneza mazingira hasi ya mawazo na hisia hasi au muingiliano na mambo yasiyojenga halafu utegemee nafsi yako itajiachilia. Nafsi yako itajenga ukuta wa kujihami maana ndivo mwanadamu alivo kiakili katika maisha yanayoonekana kama mapambano.

Pia usipende kuipa nafsi yako maumivu yasiyokuwa na sababu na mara nyingi pale akili yako inaposhindwa kuendana na misingi ya nafsi yako. Na usipende kuipa nafsi yako vifungo kwa kufuata njia ambazo unajua nafsi yako haiwi huru kuchanua.

No comments:

Post a Comment