Sunday, April 23, 2017

TAFUTA AMANI YA NAFSI

Hakuna jambo lenye msingi katika uimara na utashi wa nafsi kama amani ya nafsi - Nickvaleries

Huwezi kukua katika utashi wa nafsi pasipo kuwa na amani ya nafsi. Imani ikikaa katika nafsi humuwezesha mtu kustahimili misukosuko ya nje kwasababu kinachoweza kuzamisha meli sio bahari bali maji yanayoingia ndani ya meli.

Ukiweza kuiacha nafsi yako katika usalama kwa kujenga ukuta kuzuia yale yanayotokea yasiondoe amani ya nafsi utaweza kustahimili mengi. Ukikosa amani lazima utakosa imani na ukikosa imani hata utendaji wako na maneno yako yatakwenda kinyume na uhalisia.

Jiulize ni mambo gani ambayo unayaruhusu katika nafsi yako...Je yanaimarisha ngome za utulivu wako au yanabomoa amani ya nafsi yako na kukupa hali ya taharuki. Waweza kuwa na vyote ukakosa amani na ukikosa amani ukakosa imani huweza kuwa na furaha.

Hakuna furaha mahali palipokosa amani...Huwezi kuwa na furaha ya nafsi au kufurahia yale mazuri yanayokuzunguka kama ukikosa amani.  Tafuta kuwa na amani na jiimarishe kinafsi ukiziimarisha ngome za nafsi yako.

Jitahidi kujenga ngome zenye usalama ndani yako kiasi cha kusimama imara kinafsi hata kama mazingira ni yenye taharuki..sikiliza ulimwengu una taharuki na ukikosa amani jua huwezi kuwa na furaha.

Amani inaweza patikana kwa kuimarisha misingi ya uaminifu, mawasiliano, utashi wakihisia na utu. Tambua kwamba kila jambo linafanyika kuwa jema na wewe ni mwenye hatma njema na kuna mambo mengi mazuri ambayo yako mbele yako.

Taswira yako ni ya muhimu sana ukitaka kuwa na amani. Je unaangalia nini na unasikiliza nini? Hakikisha umejiimarisha kuratibu kila kinachoingia katika nafsi yako.

Usipende kuyapa muda mwingi mawazo na mazingira yanayoondoa amani yako. Itenge nafsi yako ili iwe na amani.


No comments:

Post a Comment