Napozungumzia tabia ya ukimya nazungumzia ukimya wa nafsi na ukimya wa tabia na hata mazingira kwa ujumla. Jamii kwasasa imezungukwa na vivutio na purukushani nyingi ambazo haziruhusu au hazisababisha ukimya. Shida kubwa ni kwamba baada ya purukushani za kila siku kinachobaki katika nafsi ni upweke unaotokana na kutojenga muda muafaka kusikiliza nafsi yako na kutafakari.
Ukimya kwanza unakuwezesha kujitambua kwa kuwa utakuwezesha kujitafakari kwa utulivu vipawa na uwezo wako na kukuwezesha kufikiri kwa makini juu ya hatma ya maisha yako.Pia ukimya utakuwezesha kutambua ni maeneo gani katika maisha yako yanahitaji uangalizi ili kukuongezea thamani. Pia utakuwezesha kusikiza miongozo inayotoka ndani ya nafsi yako.
Utajua ni nini unachotaka na ni nini unachokiamini kwasababu umezungukwa na kelele nyingi za maisha...Kelele za mitazamo ya watu, maneno ya watu na hata changamoto za maisha. Usipojenga tabia ya ukimya utakuwa ni mtu mwenye hisia za upweke mara kwa mara maana muda mwingi utajikuta umeenda tofauti na nafsi yako na kufuata mvuto wa kelele zinazokuzunguka.
Kumbuka palipo na ukimya ndipo maarifa, hekima na amani ya nafsi hukaa, pia katika ukimya kunajengeka tabia ya kuwa macho juu ya mahitaji na hisia za wengine. Mahusiano ya watu ambao hawajajenga tabia hii huwa na lawama, malalamiko na mikwaruzano ya hapa na pale kwasababu ya kukosa ule muamko na kuwa macho juu ya mahitaji na hisia za wengine.
Mambo ya kufanya na kuzingatia ili kujenga tabia ya ukimya:-
1. Pendelea kuwa na tabia ya kukaa mwenyewe ukitafakari juu ya maisha yako pasipo vurugu au purukushani kutoka kwa watu wengine
2. Jenga tabia ya kutembea au kutembelea maeneo yenye utulivu na malihai kama miti, bustani nk
3. Penda kuwa msikilizaji, mtazamaji na mtu anayetafakari zaidi kwa kile anachokiona.
4. Penda kupangilia vitu vizuri maana siku zote mlundikano wa vitu hautokuruhusu kuwa na muda mzuri wa kutafakari.
5. Jenga tabia za kiimani kama kusali na kusikiza nyimbo za taratibu zenye kuinua nafsi.
No comments:
Post a Comment