Moja ya mambo ambayo unatakiwa ujijengee katika maisha yako ni kupumzisha akili yako. Akili ambayo inakosa mapumziko huwa na uzito kuchukua hatua na hata kupata majibu ya maswali yanayokuzunguka.
Kupumzika ni zaidi ya kulala au kutofanya kazi bali kupumzisha akili ni kuacha kwa muda kufanya mambo fulani au kujishughulisha kwa mambo fulani. Maisha bila mapumziko hukosa msisimko na kuna wakati utajikuta bila ari ya utendaji kwasababu hukuweza kuupa mwili na akili mapumziko.
Muda wa kupumzika sio muda wa kuendelea kutumia simu au kuangalia runinga. Unachofanya pale ni kuendelea kuishughulisha akili na kujiweka wazi kwa fikra asi zinazochosha akili. Muda wa mapumziko ni muda wa kuweka pembeni stress na mawazo juu ya misukosuko na changamoto zinazokuzunguka.
Kuna watu ambao husema kupumzisha akili hakuyafanyi matatizo yaondoke, ni kweli lakini kupumzisha akili ni kuiwezesha kupata majibu ya matatizo hayo. Usidhani kuwa kupumzika ni kupoteza muda au kuwa mzembe.
Kuna usemi unasema kuwa "more than working hard, work smart", bila akili nguvu hupotea. Lazima akili ipumzishwe ili ilete ufanisi unaotakiwa. Njia nzuri ya kupumzika ni wakati wa kukaa kufurahia uzuri wa maisha na kutafakari mema.
Maandiko husema kuwa siku ya saba Mungu alipumzika na kufurahia uumbaji wake. Wakati wa mapumziko ni wakati wa kufurahi uzuri wa maisha. Katika wakati huu iache akili yako ifurahie uzuri wa maisha na mambo mazuri. Wengine hujitenga kabisa kwa muda na watu wengine.
Ukiona unakosa furaha ya maisha na msisimko wa kazi jiulize ni wakati gani uliopumzika, ni wakati gani umepumzisha nafsi yako, mara ya mwisho kufurahia uzuri wa maisha na kutafakari mazuri ni lini?
No comments:
Post a Comment