Pasipo utaratibu mambo huenda mrama. Pasipo uongozi thabiti lazima kuwe na machafuko. Ili uweze kuwa na uthibiti katika maisha lazima kuwe na utaratibu na lazima kuwe na uongozi thabiti. Wewe ni kiongozi wa maisha yako.
Usipokuwa na uongozi binafsi na utaratibu wako wa utendaji lazima utakuwa mtumwa wa uongozi na utaratibu wa mwingine. Mikwaruzo hutokea pale mamlaka zinapokinzana. Pale ambapo kunakosekana uwiano baina ya uongozi binafsi na uongozi unaokuzunguka. Pale ambapo kunakosekana uwiano baina ya utaratibu binafsi na utaratibu unaokuzunguka.
Usipokuwa kiongozi wa maisha yako utawapa wengine fursa ya kushinikiza mambo katika maisha yako na hii itakujengea hali ya kukosa furaha kwa maana utakuwa unashindana na nafsi yako inayotaka kuwa kiongozi lakini imekosa utaratibu wa kiungozi.
Uhuru siku zote una gharama, Huwezi kuwa huru kama unaogopa gharama ya kuwa huru. Nafsi yako inataka kuwa huru lakina usipojenga utaratibu na uongozi wa ndani wa hisia na maamuzi ni vigumu sana nafsi yako kuwa huru.
Je unawezaje kujenga utaratibu na uongozi wa maisha yako:-
1. Usisimame katika msingi wa hisia: siku zote ili kuwa na utaratibu na uongozi katika maisha lazima ujenge msingi imara katika nafsi yako. Na hisia sio msingi imara maana hisia hubadilika kila wakati, huwezi kuwa kiongozi wa maisha yako kama unaenda kwa hisia. Ukienda kwa hisia utajikuta unaendelea kuvipa nafasi vitu ambavyo havitakiwi kupewa nafasi kwa wakati huo.
2. Ongeza maarifa na ufahamu : Huwezi kuwa huru na kuwa kiongozi wa maisha yako kama ufahamu na maarifa yako vina ukomo. Hakuna jambo baya kama uhuru na ujinga. Huwezi kuwa mjinga halafu ukawa kiongozi wa maisha yako. Ujinga ni utumwa ndio maana kuna maandiko yanasema Utaijua kweli nayo kweli itakufanya huru.
3. Tengeneza sheria za maisha yako: lazima utengeneze msingi mgumu tofauti na hisia. Ukishakuwa na maarifa tengeneza sheria zako mwenyewe na hakikisha huzivunji sheria hizo maana ni changamoto na itakuumiza zaidi pale unapovunja sheria zako mwenyewe.
4. Fanya vitu kulingana na vipawa na karama zako : Huwezi kuwa kiongozi bora wa maisha yako kama haujipambanui na wengine. Usiwe mtu wa kufata upepo...Zig ziglar alishawahi kusema kuwa Uongozi sio kufuata njia iliyopitwa na watu bali ni kutafuta njia yako na kuacha alama. Ukiwa mtu wa kujilinganisha na wengine huwezi kuwa na utaratibu wako mwenyewe.
5. Jiamini : Dhana ya kujiamini ni pana sana. Katika jambo lolote lile usipojiamini huwezi fanya chochote, jiamini katika maamuzi yako, jiamini katika unayofanya. Wengi wanashindwa hata kufanya maamuzi magumu kwasababu ya kukosa kujiamini. Kama unataka kuwa kiongozi wa maisha yako jiamini ikiwemo huweze kufanya maamuzi na kuwa tayari kuwajibika kutokana na maamuzi yako.
* Hakuna jambo litakalokupa amani na furaha kama kutambua kuwa una uthibiti wa maisha yako. Ni jambo litakaloongeza ari ya utendaji wako na pia kukupa morali na msisimko wa kila siku wa maisha.
No comments:
Post a Comment