Saturday, September 17, 2016

JENGA MSUKUMO WA NDANI

Binadamu yeyote hutenda mambo kutokana na msukumo fulani. Misukumo iko ya aina mbili. Kuna msukumo wa nje na msukumo wa ndani. Watu wengi hutenda mambo kutokana na msukumo wa nje ambao unahusisha mazingira fulani au faida na matokeo fulani. Sio jambo baya kuwa na misukumo ya nje inayopelekea wewe kutenda jambo lakini changamoto ni kwamba ukiwa na msukumo wa nje zaidi inaweza pelekea kuwa na mguso tofauti.

Misukumo ya nje inaweza kubadilika muda wowote na hii itakupelekea kupoteza kabisa ile ari ya utendaji. Unaposukumwa kutenda jambo kwa ajili ya faida fulani itapelekea kuwa na hamaki pale hasara inapokuja au kukosekana kwa faida husika. Ukisukumwa zaidi na mazingira jua hayo mazingira yanaweza kubadilika muda wowote mfano unaweza pangiwa kutoka Dar es salaam kwenda dodoma. Hii itakusumbua sana katika kupata uwiano wa kihisia.

Ni muhimu kujenga msukumo wa ndani uliojengwa katika msingi wa mambo matatu..Moja ni Uongozi wa maisha yako, Thamani na mwisho ni kusudi.

Uongozi wa maisha yako ni msukumo wa ndani ulio na mtazamo na uthibiti wa muelekeo wa maisha yako. Ukijua ya kwamba wewe ndio mwenye jukumu ya kutengeneza muelekeo wa maisha yako itakupa msukumo wa utendaji kwa maana utajua kila wakati kuwa unalolifanya linatengeneza muelekeo wa maisha yako.

Thamani ni msukumo wa ndani uliojijenga katika mtazamo kuwa kila jambo unalolitenda unalifanya ili likujengee uwezo na ufanisi, likufanye mtu mwenye uwezo zaidi na mwenye ufanisi zaidi...uwe mtu wa thamani na bora. Ndio maana faida kubwa katika kazi sio unachokipata baada ya kazi bali ni unavokuwa baada ya kazi ( Thamani yako)

Kusudi ni msukumo wa jambo uliojijenga katika mtazamo kuwa unafanya jambo kwasababu lina maana kwako na jamii inayokuzunguka. Utasukumwa kufanya jambo kwa sababu lina maana kubwa ndani yako na kwa jamii yako.

Ukiwa na misukumo hiyo mitatu ya ndani katika kila jambo ulifanyalo, kila siku utakuwa na ari na msisimko kufanya mambo na hautopoteza hamu ya kuamka asubuhi kuiendea siku kwa furaha.

No comments:

Post a Comment