Usiruhusu yale ya jana yachukue muda mwingi wa leo- Willy rogers
Moja ya changamoto kubwa katika maisha yako ya leo ni kumbukumbu ya jana yako. Jana yako unaweza kuitumia katika tathmini yako kukuwezesha kuwa na mtazamo chanya na wa fadhila hasa ukikumbuka ulipotoka na kushukuru kwa hapo ulipo huku ukitazama unapoelekea.
Changamoto kubwa ni pale jana yako inapochukua muda mwingi kihisia na hata kimtazamo kiasi cha kukufanya kushindwa kuiishi leo yako. Jana yako inaweza kuwa mtego wako hasa pale unapokuwa na hisia zilizoshikamana na jana hiyo.
Kuna watu wengi wameshindwa kuachilia jana yao kiasi cha kutotazama fursa katika leo yao na kuacha fursa hizo zikipotea.
Wengi wameingia katika mahusiano leo na kumbukumbu la jana yao...Wengi wao wanataka kuishi leo lakini bado hawajaachana na jana yao. Ukiona unatamani sana jana ni dhahiri umepoteza dira ya leo na kesho yako. Kuna mambo mengi ya jana bado hutaki kuyaachilia na yamekuwa mzigo kwa leo yako.
Huwezi furahia leo yako kama jana yako inachukua sehemu kubwa ya moyo wako, akili yako na nafsi yako. Wengi leo wanaingia katika mahusiano huku bado hawajaacha kutazamia mahusiano ya jana yao. Wanajaribu hata kulinganisha leo na jana yao. Kuna wengine ambao pia hawajaacha machungu ya jana yafe, bado wanayapa nafasi katika akili yao kufikia hatua ya kuteswa na hofu ya kuishi leo katika ukamilifu.
Sikiza leo haiwezi kuja kama jana haijafa, Kesho haiwezi tokea kama leo haijaisha. Acha kuchelewesha furaha ya leo, fursa ya leo, nuru ya leo kwa kuendelea kukaa katika giza la jana..Weka pembeni na uiishi leo yako kwa furaha. Acha ya jana yawe ya jana...Ganga ya leo.
No comments:
Post a Comment