Imani ni kuwa na hakika ya mambo yasiyoeleweka au ambayo hayajabainishwa kwa wakati huo. Imani hukupa nuru ya kutambua mafumbo ya kinafsi na maswali yasiyo na majibu yenye kuleta taharuki katika nafsi.
Nafsi inaweza kupitia mambo fulani ambayo yanaikosesha amani na kuifanya ibaki katika hamaki kutojua ni nini kinachofuata au nawezaje kutoka katika hali fulani ya mkwamo wa kihisia au kimtazamo na kiakili. Hapo ndipo imani huja kuleta amani.
Imani inatakiwa iongoze hisia na iziweke katika hali ya utulivu. Ni vigumu kupata tulizo la kihisia bila kuweka mfumo bora wa kiimani, Ukitazamia kutoka katika mkwamo huo, ukitazamia utulivu wa hisia na ukitazamia uzuri na mambo mema yajayo.
Muda wote imani hujengeka katika msingi imara wa hatma ya kesho yenye furaha, faraja na uzuri na pia hujengeka katika faida ya leo katika mazingira hayo magumu. Imani hutazama fundisho, hutazama uzuri na hutazama uimara unaotokana na ugumu na changamoto husika.
Siku zote ukitaka kuwa na amani katika nafsi yako boresha mfumo wako wa imani, boresha mfumo wako wa kuamini, jikite katika kutengeneza imani zenye tija, imani zenye kukujenga na kukuimarisha. Na ukishapata msingi husika iache imani hiyo iamuru hisia zako zitii.
Imani ikisema nitatoka katika hii hali, ikasema nitavuka katika hili daraja la maumivu, ikasema nitapata kilicho bora, Hakuna hisia ya maumivu itakayoweza kukushikilia kwa muda mrefu au hata kukuzamisha. Utakuwa ni mtu mwenye amani muda wote.
Thibitisha imani zako kwa kuzipa msingi imara kwa kuzifanya sheria za nafsi yako. Imani juu ya uzuri wako, imani juu ya stahiki yako na yale unayoyatarajia na yenye kukupa amani ya nafsi, hakikisha unajijenga na kujithibitisha katika imani hizo kwa kusimama bila kuyumba kama hisia za taharuki na uchungu zikija.
Huwezi kuwa na amani ya nafsi kama huna imani na hali fulani, kama huna imani na jambo fulani, kama huna imani na watu fulani. Ni vyema ukajiimarisha katika imani na siku zote hakikisha imani yako inajengeka katika kweli. Huwezi jenga imani kwa kitu cha uongo. Imani lazima isimame katika misingi ya kweli, fikra chanya, ubora wa nafsi na utu.
No comments:
Post a Comment