Monday, May 15, 2017

CHUNGA MOYO WAKO

Chunga moyo wako maana hiyo ndiyo bustani ya amani na furaha yako. Nafsi yako hustawi katika bustani ya moyo wako. Katika bustani ya moyo wako kunaweza kuwa na maua ya furaha, amani na faraja au magugu ya maumivu na uchungu. Kuwa muangalifu sana kwa kuchunga moyo wako kila wakati ni nini kinachoota.

Kuna mawazo na maneno ambayo ukiyaruhusu yaingie moyoni yanaenda kuweka majeraha ambayo kupona kwake kutakuchukua muda sana. Majeraha hayo yatajenga mfumo wa kifikra wa kujihami ili kuzuia maumivu mengine. Hasara ya fikra za kujihami ni kwamba utashindwa kufurahia uhuru na uzuri wa maisha kwa kuwa utaishi kwa kujihami.

Moyo wako unatakiwa ulindwe kama ngome imara. Ukiruhusu maumivu au matatizo yakaingia katika bustani ya moyo wako yataenda kuotesha magugu ya mawazo na fikra hasi. Kuna maneno ukiyaruhusu kuingia siku moja yatautesa moyo wako wakati wote. 

Safisha moyo wako kwa kuondoa yale ambayo yanauumiza na kutesa moyo wako. Yale ambayo kila ukiyafikiria unasikia kama kichomi ndani ya moyo wako, yale ambayo kila ukiyapa nafasi katika akili yanakububujisha machozi ya uchungu moyoni mwako.

Tambua kuwa moyo wako unatakiwa kustawisha amani, furaha na upendo. Ukiwa na moyo wenye uchungu inageuka kuwa sumu inayodhoofisha nafsi yako na akili yako. Utakuwa mtu mwenye vifungo badala ya uhuru.

Chunga moyo wako na uache katika amani. Usiuache umekaa katika dimbwi la maumivu au usiuache ushikilie uchungu unaokuumiza, usiuache ushikilie maneno makali au misumari ya mitazamo hasi juu yako. Usiruhusu moyo wako udunde kwa kasi kwa kukosa amani au kuwa na taharuki, Jipe utulivu kwa kuruhusu uzuri na furaha istawishe moyo wako.

Ruhusu yale yenye furaha na amani na yenye uzuri na utulivu ndio yakae katika moyo wako. Stawisha moyo wako ili ukutunze na uachilie yale yenye furaha, amani na pumziko. Kama vile damu inavoingia na kutoka katika mkondo wa mishipa ya damu, wewe pia tengeneza mkondo wa kuingiza furaha nyingi, amani nyingi na faraja nyingi moyoni mwako kwa kukaa na watu au mazingira yatakayosaidia hivo vitu lakini ondoa moyoni mkondo wa maumivu, uchungu na yale yanayoutatiza moyo

Lazima kuwe na uwiano baina ya yanayotoka na yanayoingia, usipende kuingiza mawazo hasi, Itafute hiyo furaha na amani ili ustawishe bustani ya moyo wako.

Fikra chanya au mazingira chanya sio tu yale yanayokusukuma kufanikiwa bali pia kuustawisha moyo wako na kuuacha katika hali ya utulivu.

No comments:

Post a Comment