Thursday, May 25, 2017

KUTOKA KATIKA UCHOVU WA KINAFSI

Uchovu wa kinafsi ni hali ya nafsi ya mtu kukosa nguvu ya kusimama ili kuweza kuhimili mitikisiko hasi. Ni hali ambayo kama ikiingia humjenga mtu kutaka ukombozi wa kinafsi na pumziko.

Kila uchovu unahitaji pumziko lakini njia za kupata pumziko ina utofauti. Kuna pumziko la kudumu na lile lisilo la kudumu. Watu wengi wamekuwa wakishindwa kutofautisha mapumziko hayo kutokana na kukosa taswira hada hasa pale uchovu unapokuwa mkubwa.

Changamoto kubwa ni uchaguzi wa pumziko la nafsi yako maana waweza fanya uchaguzi wa kudumu au wa muda mfupi ambao utakupa uchovu mkuu baada ya ganzi ya pumziko hilo kuisha.

Ili uweze kuchagua pumziko la kudumu ni lazima ujue chanzo kikuu cha uchovu wako wa kinafsi maana vichocheo vya uchovu huo mara nyingi ni kama mchwa ambao hukula taratibu nguvu yako ya kinafsi na kukuacha mchovu.

Unaweza pata uchovu wa kinafsi pale unapojaribu jambo linashindikana au pale unapotaka kubadili jambo inashindikana, unapotaka kubadili hali fulani lakini inashindikana au inaweza ikawa jambo fulani linakushambulia kila wakati ambalo unajaribu kuliepuka, au yawezakana ni watu ndo wanakupa uchovu wa kinafsi pale wanapoila amani yako, wanaposhambulia nguvu yako ya kusimama, na kutenda yale yanayovuruga misingi yako. Unaweza pata uchovu wa kinafsi na pengine ukajaribu kupata pumziko lakini ukashindwa katika uchaguzi wako ni lipi pumziko hasa unalohitaji.

Ukishindwa kujua hasa ni pumziko gani unalohitaji waweza jikuta unapata pumziko la muda mfupi ambalo likawa kama kilevi cha nafsi kisichokupa suluhisho la kinafsi la kudumu bali kinakupa nafuu ya muda mfupi tu.

Ukitaka kuondoa uchovu wa kinafsi siku zote jaribu kujitia nguvu kwa kuelekea zaidi pale ambapo panakutia nguvu, panakupa amani, panakupa mguso chanya, pana uwiano na kile unachokiamini, na pana misingi ya kiutu yenye uhusiano na nafsi yako.

Uchovu wa kinafsi humkuta kila mtu kwa wakati fulani lakini tofauti inakuja katika uchaguzi wa mapumziko. Waweza jikuta unajiingiza katika pumziko la muda mfupi ambalo badala ya kuitia nguvu nafsi yako linazidi kukudhoofisha.

Chagua vyema pumziko la nafsi yako ili uweze kuushinda uchovu wa kinafsi.

No comments:

Post a Comment