Moja ya changamoto katika maisha ni pale tunaposhindwa kutengeneza mkondo mzuri wa mawasiliano na hii upelekea mikwaruzano na hata hali ya taharuki na hata hali ya mashaka juu ya mustakabali mzima wa mambo.
Mahusiano pasipo mawasiliano mazuri ya kinafsi ni chanzo kikubwa cha huzuni na hata kuumizana, waweza kuwa na nia njema lakini ukishindwa kutengeneza mkondo mzuri wa mawasiliano unaweza eleweka vibaya. Au unaweza kumuumiza mtu mwingine, ni muhimu sana ukawa mtu wa kuwa unazungumza.
Ni lazima ujenge hali nzuri na msingi imara ili uweze kuwasiliana na mwenzako au yule ambaye unataka kuwasilisha kile unachoona kinakutatiza. Wakati mwingi huwa tunadhani kwamba ni lazima tutafute misamiati mizuri ya mawasiliano, ni kweli pia kuna wakati unaweza kuwasilisha jambo fulani likapokelewa usivyodhania ndo maana kuna wakati unaweza kuwa na hofu fulani.
Ni muhimu kujenga msingi wa uwazi na ukweli na uwe huru maana pasipo uhuru wa nafsi juu ya jambo fulani huwezi kujenga mkondo mzuri wa mawasiliano ndio maana ni muhimu kuwa na msingi mzuri wa kihisia ukitaka kuwa na mkondo mzuri wa mawasiliano...Tambua ya kwamba unapokuwa huru kuzungumza ndio utakuwa na uhuru wa kuwa vile unavotaka.
Kuna sauti nyingi ambazo zinaweza kuja katika akili yako kukuzuia kujenga mkondo mzuri wa mawasiliano, kukosa amani ya nafsi, hofu au hata kutotaka kufikiriwa au kutazamiwa vibaya ndio maana inakupasa uwe na uhuru na amani ya nafsi na utambue kuwa wewe ni nafsi huru na unatakiwa uwe huru kuwasilisha yaliyo katika nafsi yako.
Jifunze kuzungumza kama unadhani huwezi kuzungumza yaliyo ndani ya nafsi yako, tambua nafsi yako ina uzuri na ukuu ambao kama ukishindwa kuzungumza inakuwa vigumu kueleweka....iache nuru yako ing'ae...usihofie kuzungumza. Usipozungumza unaweza jikuta upo katika hali ya taharuki na ukaishi kama mfungwa wakati ukisema ukweli utakuwa huru
Hekima ni kutambua njia na muda muafaka wa kuzungumza lakini mawasiliano ya nafsi ni jambo la msingi sana, yatakuweka huru. Ukitaka sana kufurahisha watu pia inaweza kuwa changamoto yako kuzungumza, pia usipotaka kuwaumiza watu inaweza kuwa changamoto yako kuzungumza lakini ni vyema ukawa huru katika nafsi.
No comments:
Post a Comment