Moja ya changamoto kubwa ambayo watu wengi huwa tunayo ni kutofahamu nini tunachotaka au tunachohitaji katika maisha. Watu wengi hudhani wanajua wanachokitaka au wanachokihitaji lakini ukiangalia matendo yao utatambua kuwa wengi hawajui wanachokitaka katika maisha. Usipojua unachotaka katika maisha utakuwa ni mtu wa kuzunguka zunguka kujaribu jaribu kila kitu kuona kina mguso gani kwako.
Kuna dhana nyingi sana ambazo tunazo ju ya yale tunayotaka katika maisha na unaweza ukapewa kila ulichodhani unakitaka kisha ukaja kugundua kuwa bado kuna kitu kingine unachokitaka. Na utakuwa ni mtu usiye na furaha wala amani kwasababu hujui unachokitaka. Pengine hata ukawa mtu mwenye lawama katika kila jambo kwasababu wewe mwenyewe hujui unachokitaka.
Pengine pia unaweza jua unachokitaka lakini unadhani ni jambo la kufikirika, huo mtazamo unaweza kukufanya ukaendelea kuwa kama mtumwa anayezunguka jangwani asijue anapoelekea. Kuna mwanafilosofia mmoja aliwahi kusema kuwa Watu wengi hawajui wanachokitaka hadi uwaonyeshe wanachokitaka. Ni muhimu sana kujua unachokitaka.
Njia pekee ya kujua unachokitaka ni kujitathmini nafsi yako na kujitambua utu wako ndipo utajua ni nini unachohitaji. Mwanafilosofia mmoja aliwahi kusema kuwa kama hakuna adui ndani adui wa nje hawezi kutudhuru. Nafsi yako ya ndani imeundwaje? Pengine ushawahi kujiuliza ni jambo gani linakupa amani na unaamini ndio jambo ambalo ukilipata kama msingi wa maisha yako utaweza kupata mambo mengine yote?
Kila nafsi inahitaji uhuru na amani na furaha na wengi wetu tumedhani tukipata vitu basi nafsi yetu ndo itakuwa imepata inachotaka. Hapana!! Nafsi yako inahitaji kukua na jambo lolote linaloweza kuinyanyua nafsi yako ndilo jambo unalohitaji. Nafsi yako inahitaji thamani na jambo linaloweza kuipa thamani nafsi yako ndilo unalohitaji. Nafsi yako inahitaji amani na jambo lolote linaloweza kukupa amani ya nafsi ndilo unalohitaji.
Ukishajua msingi hasa wa mahitaji ya nafsi yako itakuwezesha kutambua ni nini unachohitaji katika maisha, iwe ni katika uchaguzi wa kazi, iwe ni katika mahusiano au nyanja yeyote ya maisha. Utatambua marafiki wa nafsi yako, utatambua hata mwenzi wa nafsi yako, utatambua hata kusudi la maisha yako.
Asante kwa kutoa mada nzuri..
ReplyDeleteAsante kwa kutoa mada nzuri..
ReplyDelete