Tuesday, October 25, 2016

UTUMIE VEMA MUDA WA KUSUBIRI

Moja ya changamoto katika maisha ni pale ambapo matarajio yetu yanachelewa, pale ambapo unasubiri jambo fulani likamilike. Ni sawa na kupanda mbegu chini ya ardhi na kusubiri mti uchipuke. Muda mwingi tumekuwa tukiona wakati huo ni mrefu na hata kuingiwa na hisia za huzuni na kuchoka pale tunapoona matokeo yamekawia.

Inapaswa ujifunze kuwa wakati wa kusubiri huwa mrefu na wenye uchungu pale ambapo kwa muda huo unasimama katika mambo mengine huku ukisubiria. Hata mkulima huwa akipanda mbegu hakai akisubiria. 

Jizamishe katika mambo uyapendayo hadi usahau kuwa ulikuwa unasubiria jambo fulani.
Subira yenye furaha ni ile subira ambayo unaifanya huku unaendelea kufanya mambo uyapendayo. Hata katika mahusiano yakupasa kuwekeza pia kuhusiana na nafsi yako wakati uko katika mahusiano na mtu mwingine, mahusiano haimaanishi uiache nafsi yako katika ukame ukisubiria muitikio wa nafsi unayohusiana nayo.

Mfano umepanga kukutana na mtu na hajafika huwa unafanya nini huku ukisubiri?, mfano upo katika foleni sehemu huwa unafanya nini ukisubiria?, mfano umeingia katika mgahawa chakula kimechelewa huwa unafanya nini ukisubiria? Dunia haitakiwi kusimama wakati wewe ukisubiria muitikio wa mtu au jambo. Endelea kufurahisha nafsi yako kwa kufanya yale uyapendayo la sivyo utakuwa unaingiwa na huzuni ukiona jambo linachelewa.

Unasubiri jambo gani katika maisha, iwe katika mahusiano au eneo lolote, usisimamishe dunia ya nafsi yako ukisubiria, kuna mambo mengi unaweza kufanya wakati unasubiria kuna vitabu hujasoma, kuna tabia na vipawa unaweza vikuza, kuna marafiki unaweza wasiliana nao, unaweza kwenda kutembea. Kuna mambo mengi nafsi yako ingependa kuyafanya na bado hujayafanya...tumia huo muda.

Jifunze pia kutembea na kitabu kidogo cha kunakiri mambo au yafundishe macho yako kuona uzuri wa mambo yanayokuzunguka, jenga akili ya kudadisi, andika mambo unayoyaona, changamoto mbalimbali, sikiliza audio za kukujenga, waweza enda kusaidia mtu mwingine, tembelea marafiki na jamàa na mzungumze, kuna sehemu unaweza itajika kusubiri muitikio wa jambo fulani, wewe endelea kuishi dunia iliyomo nafsini mwako.

Hata katika mahusiano watu wamekuwa wakilaumiana kwakuwa husubiri miitikio ya watu fulani lakini huchelewa kuitikia, wakati unasubiri waweza fanya mambo mengine, waweza andika mambo yanayokufurahisha katika mahusiano nk, jizamishe katika mambo ya nafsi yako na vipawa vyako, wekeza katika ufahamu wako.

2 comments: