Moja ya changamoto tunazopitia katika maisha ni hofu ya kukutana na hofu zetu na hofu ya mguso utakaotokana na hofu zetu. Huwezi kuwa huru kutoka katika hofu unayohofia kukutana nayo. Siku zote kuwa tayari kukutana na hofu zako na jivike ujasiri wa kuweza kuzidhibiti hofu zako.
Katika maisha lazima uwe na ujasiri wa kusonga mbele na kujua kuwa iko siku utakutana na hofu zako. Lazima ujipange jinsi ya kukabiliana na hofu yako na uwe jasiri maana hofu yako siku zote ndio gereza lako. Kuna wakati katika maisha inakubidi kuvuka daraja lenye kutia hofu kwa ujasiri ukitazamia maono uliyonayo katika maisha.
Amani ya nafsi ikishakaa ndani yako itakupa ujasiri wa kukabiriana na hofu yako ndio maana mwanafilosofia mmoja aliwahi kusema kuwa kama hakuna adui ndani ...adui wa nje haweza kutuathiri. Na hapa anapozungumzia adui sio lazima awe adui anayekupinga bali kuna maadui wa furaha yako na maono makubwa ambao wanaweza kuja kama watu wa karibu wakikushauri au mazingira fulani yakikukwamisha.
Lazima ujivike ujasiri na useme kwa jambo lolote nitasonga mbele na niko tayari kukutana na hofu yangu. Bila kuwa na huo ujasiri hofu yako itaendelea kukuzuia kusonga mbele. Na njia pekee ya kuweza kuishinda hofu yako ni kuwa mkweli kwa nafsi yako, kuwa mkweli kwa kile nafsi yako inataka na pia kuikubali amani iliyo ndani yako maana amani ya nafsi siku zote ni ya msingi sana. Ukisha kuwa mkweli uweke wazi ukweli ulio ndani yako, usiuogope, wala usiogope jinsi watu watakavoupokea huo ukweli.
Njia ya maisha siku zote ni ya kufanya maamuzi na kusonga mbele. Muda wa kukaa kutafakari kwa sababu ya hofu iliyo mbele yako ni kujikwamisha mwenyewe. Songa mbele kama una imani na kweli iliyo ndani yako. Amini tu kwamba kila jambo linafanyika kuwa jema. Maamuzi siku zote hutujenga, pasipo maamuzi tutaendelea kukaa katika hali ya mazoea ambayo pengine yangekuja kutuumiza.
Kuwa jasiri na Hofu zako zitakimbia. Usipokuwa jasiri hofu zako zitaendelea kukufunga sehemu ulipo.
Im inspired..
ReplyDelete