Imani mara nyingi hutokana na uzoefu juu ya jambo fulani, uzoefu huo hujiimarisha katika ubongo wako na kutengeneza mfumo wa kisheria ambao utatawala mitazamo yako na utakujengea kawaida yako. Na mara nyingi kawaida hiyo hujenga utamaduni ambao utakusanya mambo ya kuthibitisha na kuendana na utamaduni huo.
Unapojenga imani fulani siku zote imani hiyo huvuta mazingira husika ya kuthibitisha imani hiyo. Mfano unapojenga imani kuwa katika mahusiano jinsia fulani sio ya kuaminika imani hiyo huvuta mazingira hayo, imani hiyo itakuongoza kuchagua watu wasioaminika na hata itakujenga kutafuta mazingira yasio aminifu katika mahusiano yako ili kuthibitisha imani hiyo.
Siku zote akili hujisikia furaha pale inapothibitisha mitazamo yake na malengo yake..ndio maana siku zote ukithibitisha jambo ulilokuwa na wasiwasi nalo hata kama linaumiza akili yako itasema nilijua tu....tafsiri ya neno nilijua ni kuipa thamani akili yako kwa uthibitisho huo na kuijengea thamani kwa imani hiyo.
Ni muhimu utambue kuwa unatakiwa kutafakari sana kabla hujakiweka kitu kama imani yako kwasababu imani hiyo itakutengenezea kawaida yako. Na siku zote kawaida yako ndio ulimwengu wako. Watu wengi wamejijengea kawaida mbaya hadi pale jambo zuri linapokuja wanalikataa na kuliona haliwastahili. Kuna watu wamejijengea kawaida kiasi cha kwamba jaribio lolote la kutoka hapo ni maumivu kwao.
Usijenge msingi wa kiimani ambao unaona kabisa ni asi kwasababu huo msingi utavuta mazingira ya kuthibitisha hayo uliyoyaweka kama sheria. Hakikisha kabla hujaliamini jambo na kuliweka katika akili yako litafakari. Usije kufungwa na kawaida ambayo itakutesa. Mfano mtu anaweza akaja kukwambia yaani mie kila mahusiano yangu naumizwa...unamuuliza je unadhani kwanini....mtu anakwambia mie nadhani nina mkosi au wanaume wote ni wahuni, au wanawake wote hawaaminiki...Tayari kishajenga imani ambayo inavuta mazingira kuthibitisha imani hiyo.
Ni jambo la muhimu sana kuongeza maarifa juu ya jambo usilolijua badala ya kujijengea imani ambazo zitakujengea kawaida yako. Pia ni kubadilisha taswira yako, ni nini hasa unaangalia au ni wapi hasa mtazamo wako ulipo maana taswira siku zote hukutengenezea imani itakayokujengea kawaida itakayovuta mazingira kuthibitisha mambo husika.
No comments:
Post a Comment