Uimara wa mtu katika nafsi umejikita zaidi katika utashi wake wa kihisia. Binadamu ni kiumbe chenye nafsi na nafsi ya mtu imeundwa katika mfumo wa hisia. Hisia za mtu pia zimeundwa katika mfumo wa utu wake. Kila mtu ana muundo wake wa kiutu ambao ndio msingi hasa wa uratibu wa hisia za mtu huyo.
Hisia ni misukumo na mihemko ya kinafsi ambayo hujitokeza kutoka kipindi hadi kipindi kutokana na mabadiliko ya ndani au nje. Yaweza ikawa mabadiliko ya kimazingira au mabadiliko ya tabia za mwili. Changamoto kubwa ya hisia ni kwamba ni kama upepo, huja na kufika katika kilele lakini baadaye hushuka katika ukawaida na pengine hushuka zaidi ya hapo.
Hapo ndipo wengi hujikuta wanasema leo najihisi niko chini sana kihisia au nimezama katika hisia na hata wengi hutumia kauli za vitabu vya dini na kusema leo nimezama katika bonde la uvuli wa mauti. Lakini hao hao watu nyakati nyingine utasikia anasema leo nina msisimko au leo niko hewani. Yote hayo ni mabadiliko ya kihisia.
Hisia zinaweza kuwa nzuri kama zikitumika vizuri lakini changamoto kubwa ni pale mfumo wa uratibu wa kimaamuzi katika akili unapofungwa katika hisia ambazo zinapanda na kushuka. Kuna ambao wamekuwa na utashi wakufikiria lakini wamekosa utashi wa kihisia.
Utashi wa kihisia ni uwezo wa kuratibu hisia zako na kuzielekeza vile unavotaka. Watu wengi tumekuwa na utashi wa ki akili lakini tumekosa jambo la muhimu sana ambalo ni utashi wa kihisia kupelekea yale tunayoyajenga kwa akili zetu yanaharibiwa na hisia zetu.
Waweza fikiria jambo zuri na ukaliwekea mikakati madhubuti lakini kinapofika kipindi cha mtikisiko unaogusa hisia ,wengi wetu tumejikuta tukiruhusu hisia zetu ziharibu hata ule mtazamo chanya wa yale tuliyoyajenga kwa akili zetu.
Watu wengi waliofanikiwa au wakuu wamejikuta wakianguka na kufanya maamuzi mabovu kwasababu ya kukosa utashi wa kihisia na wamejikuta wakizama katika dimbwi ambalo pengine kusababisha zile imaya walizozijenga kwa akili nyingi kuanguka kutokana na kukosa utashi wa kihisia.
Wekeza sana kuwa utashi wa kihisia uweze kutambua ni hisia zipi zinakujenga na zipi zinakubomoa. Hisia zipi zinakuimarisha na hisia zipi zinakudhoofisha, hisia zipi zinakuinua na hisia zipi zinakuangusha. Ukiwa na utashi wa namna hiyo utaweza kuzitumia hisia hizo ziweze kukutumikia na sio wewe kutumikia hisia zako.
Je wawezaje kuwa na Utashi wa kihisia
1. Pambanua hisia zako pindi zinapokuja na utambua mlengwa wa kila hisia.
2. Tambua chanzo cha hisia husika au mifumo sababishi ya kutokea kwa hisia hizo.
3. Jifunze kuzimudu hisia kila zinapokuja kwa kuifanya nafsi yako izungumze na hisia hizo
4. Tambua kuwa hisia sio jambo baya na wala sio udhaifu bali ni muundo wa kinafsi hivo hisia zako zikubali kuwa ni zako na wewe ndio mwenye kuwajibika kwa hisia hizo. Usitafute kisingizio juu ya hisia zako.
5. Jiimarishe katika uvumilivu ili uweze kuziratibu hisia zako na kuratibu mkondo wa hisia zako maana hisia ni kama mkondo wa maji
6. Pendelea kutenga muda wako wa upekee ukizungumza na nafsi yako ili uweze kuthibitika katika uimara wa kihisia.
Hakuna jambo la msingi na lenye kufaa kama kuwa na utashi wa kihisia maana maisha yako yanaweza kuwa yenye furaha na amani au kuwa na shida na maumivu kama hauna utashi wa kihisia.