Wednesday, August 23, 2017

UDHIBITI BINAFSI

Nafsi isiyo na udhibibiti binafsi ni sawa na mji usiokuwa na kuta

Moja ya changamoto kubwa ya kinafsi ni ukosefu wa udhibiti binafsi. Udhibiti binafsi na uwezo wa kinafsi wa kuratibu na kuzuia kila ambacho kinaweza kuingia katika nafsi husika na hapo ndipo tabia ya udhibiti binafsi inapokuja. Ulimwengu ni kama jalala yenye kila aina ya mambo, yenye kuharibu nafsi, yenye kujenga, yenye kuleta tabia na mitazamo asi au chanya, hivo ukitaka usalama wa kinafsi ni lazima uwe na udhibiti binafsi.

Haijalishi kwamba umepewa macho, kinywa au masikio, uimara wako unatokana na kutumia milango hiyo katika mambo ya msingi pekee. Udhibiti binafsi sio tu kudhibiti haja za mwili wako bali pia ni kudhibiti milango inayoingiza habari ndani yako. Huwezi kuwa na uimara kama ni mtu wa kutazama kila kitu, mtu wa kusikiza kila kitu, mtu wa kuchangia kila kitu, mtu wa kufatilia kila kitu au mtu wa kuongea kila kitu, hapana. Hautakuwa mtu mwenye utashi mzuri wa kihisia na hata kiakili.

Kuna tamaa za kinafsi kama shauku ya kutaka kufahamu mambo yasiyo na tija kwako, au kutaka kusikiza maswala yasiyoongeza thamani kwako au kutaka kufatilia watu wasio katika mlengwa wa yale yanayokuhusu. Ni tamaa tu ya kinafsi kutaka kuburudishwa na yanayowatokea wengine pengine hata kama hayana faida kwako. Usichofahamu ni kwamba unaijaza nafsi yako na mambo ambayo yanaongeza mzigo au yanakupa mtazamo ambao hauna tija kwako. Hakuna changamoto kubwa kama uchaguzi. Pale unapokuwa katika mazingira yanayokupasa uchague kuburudisha nafsi au kujenga nafsi.

Tafuta burudani ya kinafsi kwa mambo yanayohusiana na mambo ya msingi yanayokujenga. Kuwa na udhibiti binafsi, na wengi ambao hawana udhibiti binafsi wamejikuta katika matatizo mengi ya msongo wa mawazo au hata mikwaruzano isiyo na tija na watu wengine. Hata kama jambo lipo mbele yako sio lazima uburudishe nafsi yako kulifatilia. Hata kama hoja iko mbele yako sio lazima kuburudisha nafsi yako kuchangia. Hata kama maneno yanasemwa juu yako sio lazima kuruhusu nafsi yako kujibu, hata kama una shauku ya kuwafatilia watu sio lazima uruhusu nafsi yako kuwafatilia. Kama jambo badala ya kukusaidia linakujaza ujinga dhibiti nafsi yako na uliache.

Hakika usipokuwa mtu wa kudhibiti nafsi yako utakuwa mtu mwenye kubeba kila aina ya uchafu.