Friday, August 26, 2016

KWANINI HATUTENDEI KAZI TUNAYOYAJUA

Changamoto kubwa tuliyonayo ni kujua sana, kusoma sana lakini hatutendi yale tunayoyajua. Ni sawa na kuingiza vitu vingi ndani yako lakini utoaji wake au utendaji wake ni mdogo. Wengi hawasongi mbele kwasababu wanajua sana lakini wanatenda kidogo.

Huwa najiuliza maswali mengi hasa pale napokijua kitu lakini nashindwa kukitendea kazi. Huwa najiuliza nini tatizo? Hasa hasa pale unapokuja kuona mtu mwingine akikitendea kazi kile ulichokijua wewe na akapiga hatua.

Hata maandiko husema muwe watendaji wa neno na sio wasikilizaji tu. Na yule ajuaye jambo na kutolitenda huhesabika kwake kama uovu.. Kwanini? Kwasababu ufahamu unapaswa kukuweka huru na sio kukufanya mfungwa. Unapojua kitu ni nafasi kwako kukifanyia kazi ili kikusaidie. Kukijua tu na kuishia pale haisaidii.

Ni kwanini watu hatutendei kazi yale tunayoyajua? Baada ya kutafakari na kuchunguza kwa makini nimekuja kugundua sababu kuu inayopelekea watu tusitendee kazi tunachokijua imefungwa katika mitazamo yetu na tabia zetu za ndani.

1. MTAZAMO BINAFSI: Hii ndiyo changamoto ya kwanza inayosababisha watu wasitendee kazi wanayoyajua. Watu wengi wana mitazamo binafsi iliyo asi ambayo hupambanua na kuua nguvu ya utendaji, ukiwa na mtazamo asi siku zote utakichambua unachokijua na kuua msukumo wako kukitendea kazi. Ni muhimu sana kujenga mtazamo binafsi ulio chanya.

2. KUKOSA UJASIRI : Watu wengi hawatendei kazi wanayoyajua kutokana na kukosa ujasiri wa kutenda. Wengi wamefungwa katika mitazamo ya watu wengine mfano ndugu wa karibu nk. Mawazo yao yakiyumbishwa kidogo wanakosa ujasiri wa kutenda. Zaidi ya vyote ni muhimu kuwa na ujasiri wa kufanya jambo hata ukikutana na vipingamizi. Lazima ujiamini katika kutenda.

3. IMANI HABA : Hili neno limekuwa lenye kufahamika sana hata katika vitabu vya dini, watu wengi hushindwa kutenda mambo kutokana na kuwa na imani isiyo thabiti. Lazima jambo unalolifahamu ulijengee msingi wa kiimani. Haiishii kulitambua bali inakupasa uliamini. Usipoliamini huwezi kulifanyia kazi

4. KUKOSA NIDHAMU: Nidhamu ni tabia ya ndani ambayo mtu huijenga. Nidhamu itakuwezesha kustahimili na kutoka katika comfort zone ( uwanda wa starehe) na kustahimili misukosuko na kuweza kusonga mbele. Nidhamu itakulazimu kufanya jambo hata usilojisikia kulifanya huku ukiwa na taswira ya matokeo chanya.

5. KUKOSA MIFUMO YA UTENDAJI: Hii ni changamoto kuu hasa pale unaposhindwa kuandaa mifumo ya utendaji kuhamisha nadharia kuwa vitendo. Mifumo ya utendaji ni malengo, muda, nguvu na uwezeshaji mwingine. Usipojenga mifumo bora ya utendaji itakuwia vigumu kutenda yale unayoyajua. Yakupasa uwekeze zaidi.
Pasipo kutathmini kwa makini hizo sababu tutaendelea kuwa watu wa kujua mambo pasipo kutenda.

No comments:

Post a Comment