Uhuru wa kihisia ni pale unapoweza kudhibiti na kuelekeza hisia zako katika muundo na mpangilio uutakao. Hili si jambo rahisi kwa maana hisia huja kutokana na mabadiliko ya ndani ya mwili na hata hujengeka katika msingi wa nafsi ya mtu hivo uhuru wa kihisia unawezekana pale tu unapojenga tabia inayoitwa Nidhamu.
Nidhamu itakuwezesha kudhibiti hisia zako kwa namna kwamba utaweza kuzielekeza au kuamua muitikio na hata namna ya kukabili hali fulani zinazojitokeza. Uhuru wa kihisia kwanza unajengwa na kuitambua nafsi yako....nguvu na mapungufu yake kisha kujenga msingi wa kimaamuzi unaotokana na sheria utakazozijenga katika akili yako.
Hisia ni kama upepo, huja na hupoa na pengine hata kupotea kabisa, upepo huo unaweza kuwa kimbunga kwako au unaweza kuwa kama kipupwe kutokana na misingi ya kinidhamu ulioijenga katika nafsi yako ambayo inakupa uhuru wa kuamua jinsi hisia zako zinavodhibitiwa. Kudhibiti hisia ni sawa na kujenga mifereji ili kudhibiti mikondo ya maji isilete madhara au isielekee kusikotakiwa.
Ukiwa mfungwa wa hisia inamaana utendaji wako au muitikio wako katika mambo utatokana na msukumo wa hisia ulizonazo. Umeshawahi kuwa hisia nzito juu ya mtu fulani au jambo fulani kwa wakati fulani na ukatamani kulifuatilia lakini baada ya muda unapoteza hiyo hisia? Na hii hasa ndio changamoto ya kufanya maamuzi kwa kufuata hisia.
Jenga utaratibu wa kinidhamu wa kuratibu hisia zako kisha zielekeze kuongeza msukumo ktk sheria ulizozijenga na wala usiruhusu hisia zako zikuelekeze kupingana na sheria zako...namaanisha usiruhusu hisia pinzani zipate nguvu. Hisia zote zielekeze unapotaka ziende. Na hii inahitaji mazoezi.
Warren buffet aliwahi kusema kuwa mtu asiyeweza kudhibiti hisia zake hawezi kudhibiti pesa zake. Na hilo ni jambo la kweli kabisa, usipoweza kuwa nidhamu ya kihisia huwezi kuwe na nidhamu ya kiuchumi
Pia usipokuwa na uhuru wa kihisia utakuwa mhanga wa maumivu mengi ikiwemo mahusiano au hata namna watu wanavoleta upinzani katika maisha yako. Watu wasio na uhuru wa kihisia mara nyingi hushindwa kuchanganua ni aina gani ya mahusiano ni mazuri kwao na yatakayowajenga, kwao hisia zikishatawala wanashindwa hata kuruhusu akili zao kuchanganua.
Maisha bila uhuru wa kihisia ni kama msitu maana kila aina ya mabadiliko yatakuwa na mguso kwako na utataka kuitikia kila ambavyo hisia zitakutuma. Lazima uwe huru kuzidhibiti hisia la sivyo zitakuzamisha.