Friday, October 28, 2016
IMANI YAKO HUJENGA KAWAIDA YAKO
Tuesday, October 25, 2016
UTUMIE VEMA MUDA WA KUSUBIRI
Sunday, October 23, 2016
TENGENEZA MKONDO MZURI WA MAWASILIANO
Moja ya changamoto katika maisha ni pale tunaposhindwa kutengeneza mkondo mzuri wa mawasiliano na hii upelekea mikwaruzano na hata hali ya taharuki na hata hali ya mashaka juu ya mustakabali mzima wa mambo.
Mahusiano pasipo mawasiliano mazuri ya kinafsi ni chanzo kikubwa cha huzuni na hata kuumizana, waweza kuwa na nia njema lakini ukishindwa kutengeneza mkondo mzuri wa mawasiliano unaweza eleweka vibaya. Au unaweza kumuumiza mtu mwingine, ni muhimu sana ukawa mtu wa kuwa unazungumza.
Ni lazima ujenge hali nzuri na msingi imara ili uweze kuwasiliana na mwenzako au yule ambaye unataka kuwasilisha kile unachoona kinakutatiza. Wakati mwingi huwa tunadhani kwamba ni lazima tutafute misamiati mizuri ya mawasiliano, ni kweli pia kuna wakati unaweza kuwasilisha jambo fulani likapokelewa usivyodhania ndo maana kuna wakati unaweza kuwa na hofu fulani.
Ni muhimu kujenga msingi wa uwazi na ukweli na uwe huru maana pasipo uhuru wa nafsi juu ya jambo fulani huwezi kujenga mkondo mzuri wa mawasiliano ndio maana ni muhimu kuwa na msingi mzuri wa kihisia ukitaka kuwa na mkondo mzuri wa mawasiliano...Tambua ya kwamba unapokuwa huru kuzungumza ndio utakuwa na uhuru wa kuwa vile unavotaka.
Kuna sauti nyingi ambazo zinaweza kuja katika akili yako kukuzuia kujenga mkondo mzuri wa mawasiliano, kukosa amani ya nafsi, hofu au hata kutotaka kufikiriwa au kutazamiwa vibaya ndio maana inakupasa uwe na uhuru na amani ya nafsi na utambue kuwa wewe ni nafsi huru na unatakiwa uwe huru kuwasilisha yaliyo katika nafsi yako.
Jifunze kuzungumza kama unadhani huwezi kuzungumza yaliyo ndani ya nafsi yako, tambua nafsi yako ina uzuri na ukuu ambao kama ukishindwa kuzungumza inakuwa vigumu kueleweka....iache nuru yako ing'ae...usihofie kuzungumza. Usipozungumza unaweza jikuta upo katika hali ya taharuki na ukaishi kama mfungwa wakati ukisema ukweli utakuwa huru
Hekima ni kutambua njia na muda muafaka wa kuzungumza lakini mawasiliano ya nafsi ni jambo la msingi sana, yatakuweka huru. Ukitaka sana kufurahisha watu pia inaweza kuwa changamoto yako kuzungumza, pia usipotaka kuwaumiza watu inaweza kuwa changamoto yako kuzungumza lakini ni vyema ukawa huru katika nafsi.
Monday, October 17, 2016
BADILI TASWIRA WAKO
Changamoto kubwa katika maisha ni kuwa na mitazamo mibovu. Taswira uliyonayo juu ya mambo inatokana na hazina uliyoweka moyoni mwako. Jinsi unavowekeza ndani yako ndo jinsi unavojenga taswira nzuri katika maisha yako. Mambo unayoyaona mazito kwako inatokana na nguvu au hazina uliyowekeza ndani yako.
Usipowekeza katika kukua siku zote hautakuwa mtu mwenye taswira nzuri....ukiwa na hazina ndogo au nguvu ndogo ya kiroho siku zote taswira yako itakuwa na tatizo...na ukikosa taswira nzuri utakuwa ni mtu mwenye kulaumu na kuona kama maisha hayakutendei haki. Maisha yapo siku zote lakini wenye nguvu ndio wanaoweza kustahimili hivo wekeza kuwa na nguvu katika nafsi yako.
Chukua kila tatizo linalokuja kwako na ulione kama jiwe la kwenda kiwango kingine. Chukua maumivu na uyaone kama fursa ya kujiimarisha zaidi roho yako. Usilalamike, wewe ni kiongozi wa maisha yako na kila jambo hufuata mkondo unaouweka wewe. Hukuzaliwa umfurahishe kila mtu hivo acha kufungwa katika mawazo au shuruti za watu. Unatakiwa uwe huru.
Ili taswira yako iwe nzuri ibadilishe, unapokuwa unatafuta taswira ya picha na camera lazima uhakikishe picha ya maisha yako unaiweka katika mraba, kuna vitu vya kuondoa katika taswira hiyo, unaweza kubadili umbali nk. Vivyo hivo katika maisha yako ukitaka upate taswira unayoitaka kuna watu inabidi uachane nao, kuna mambo inabidi uachane nayo, kuna vitu inabidi uviondoe katika taswira. Haijalishi vikoje kama unaona havipo katika taswira yako yakupasa uviondoe.
Usipokua, siku zote taswira yako itakuwa ndogo, kuna mambo mengine hujayajua au kuna mambo mengine huyaoni kwasababu huna taswira nzuri na hii hutokana na kutokuwa na hazina na nguvu ndani yako.
Thursday, October 13, 2016
SAUTI TATU KATIKA MAHUSIANO
Mahusiano yetu huguswa na sauti ambazo zinaleta changamoto na ni sauti ambazo zinamchango katika uimara wa mahusiano yako au kuanguka kwa mahusiano yako. Bila sauti hizo kuwa katika uwiano sawa basi sauti moja ikiizidi nyenzake inaweza sababisha changamoto.
Sauti hizo zimegawanyika katika makundi matatu, ya kwanza ni sauti ya nafsi ; Hii ni sauti ambayo kila mtu anakuwa nayo kiasili nayo ni sauti ya uhuru, furaha na amani. Kila nafsi inataka kuwa katika uhusiano ambapo itakuwa huru na yenye furaha na amani, sauti hii inalia kutoka ndani ya nafsi ya mtu na ndio maana kuna ambao husema kuwa katika uhusiano ambao utakuwa huru na mwenye furaha na amani.
Sauti ya pili ni sauti ya Jamii; hii ni sauti inayotoka katika jamii inayotuzunguka juu ya mahusiano yetu. Hii sauti inaweza ikawa sauti ya wazazi au sauti ya malezi na makuzi ambayo tumeyapitia. Sauti hii mara nyingi hutuambia kuwa ni nani anatufaa, au ni nani tunatakiwa tuwe naye au ni mahusiano gani ambayo inabidi tuwe nayo.
Sauti ya tatu ni sauti ya akili zetu; Binadamu huwa na hali ya kupenda kutafakari na kutumia akili katika kufanya maamuzi na pengine kuna wakati hutumia zaidi akili katika mambo fulani juu ya nini hasa jambo sahihi la kufanya.
Ili kujenga uhusiano imara lazima hizi sauti ziwe na uwiano...sauti ya nafsi inabidi iwe kama msingi itakayobeba sauti nyingine zote. Sauti ya nafsi ikizifunika sauti nyingine zote unaweza pelekea kufanya mambo ambayo yanaweza kutokubalika katika jamii na ukajikuta unakosa kabisa ushirikiano na wengine lakini sauti ya jamii ikiizidi sauti ya nafsi utajikuta unaingia katika mahusiano ambayo katika jamii unasifika lakini ndani ya nafsi yako unakosa furaha na unakuwa na upweke ambao jamii haiwezi kukusaidia.
Pia inakupasa sauti ya nafsi iwe na uwiano na sauti ya akili ili akili yako iweze kuwekeza zaidi...maana nafsi na akili zikiwa na uwiano ile amani na furaha hudhiirika katika fikra za ubunifu zaidi katika kuimarisha mahusiano hayo.
Kama unaona sauti ya jamii ni kubwa na inakutisha hakikisha sauti ya nafsi na sauti ya akili vinaungana kuishurutisha sauti ya jamii itulie.
Changamoto na jambo la msingi kwa kila mtu ni kuhakikisha hizo sauti zina uwiano ili kujenga mahusiano imara.